Hamia kwenye habari

DESEMBA 2, 2019
TOGO

Mafuriko Makubwa Nchini Togo

Mafuriko Makubwa Nchini Togo

Mvua kubwa zilizonyesha kwa muda mrefu nchini Togo katika msimu wa mvua wa mwaka 2019 zimesababisha uharibifu mkubwa nje ya mji wa Lomé, Togo. Wahubiri 257 kutoka makutaniko 7 waliathiriwa na mvua hizo. Ofisi ya tawi inaendelea na jitihada za kutoa msaada.

Katika baadhi ya maeneo yaliyoathiriwa, kimo cha maji yaliyoingia ndani ya majengo kilifikia mita moja, hivyo iliwalazimu ndugu na dada zetu kuhama nyumba zao. Wahubiri walio katika maeneo ya karibu waliwakaribisha nyumbani kwao na kushughulikia mahitaji ya akina ndugu waliolazimika kuhama.

Maji ya mvua yalichafua vyanzo vya maji katika eneo hilo. Halmashauri ya Tawi ya Benin, inayosimamia kazi nchini Togo, ilipanga kusambaza mahitaji ya msingi kupitia waangalizi wa mzunguko na wazee wa eneo hilo. Mahitaji hayo yanatia ndani dawa za kusafishia maji na dawa za kuua viini vya wadudu.

Tunasali Yehova awabariki ndugu zetu nchini Togo wanapoendelea kuonyeshana upendo wa kujidhabihu.—Yohana 13:34, 35.