Hamia kwenye habari

AGOSTI 27, 2014
TURKMENISTAN

Mama Mwenye Mtoto wa Miaka Minne Ahukumiwa Isivyo Haki Nchini Turkmenistan

Mama Mwenye Mtoto wa Miaka Minne Ahukumiwa Isivyo Haki Nchini Turkmenistan

Katika chumba cha mahakama cha muda jijini Dashoguz, Turkmenistan, Jaji Gagysyz Orazmuradov alimhukumu isivyo haki Bibi Rahmanova mwenye umri wa miaka 33 kifungo cha gereza kwa mashtaka ya uwongo. Agosti 18, Bibi, ambaye ni mama mwenye mtoto wa miaka minne, alisemekana kuwa na hatia ya “kumshambulia polisi” na pia “kufanya fujo.” a Jaji huyo alitoa hukumu kali—kifungo cha miaka minne katika gereza la wahalifu.

Akamatwa Katika Kituo cha Treni

Mambo yaliyompata Bibi yalianza jioni Julai 5, 2014, wakati yeye, mume wake Vepa Tuvakov, pamoja na mtoto wao, walipoenda kwenye kituo cha treni jijini Dashoguz kupokea machapisho ya kidini na vitu vingine vya kibinafsi kutoka kwa rafiki yao anayeishi Ashgabad. Baada tu ya wenzi hao wa ndoa kuchukua mizigo hiyo, polisi sita wanaume waliovalia nguo za kiraia waliwakamata na kuwaamuru wawaonyeshe kilichomo kwenye mifuko waliyobeba. Walipoona kompyuta na machapisho ya kidini ya Mashahidi wa Yehova, polisi hao wakawatukana na kuwatisha kuwa mtoto wao atakuwa yatima.

Bibi alianza kurekodi tukio hilo kupitia simu yake ya mkononi na kuificha ndani ya blauzi yake wakati polisi hao walipotaka kumnyang’anya. Walimvuta nywele zake, wakampiga mateke, wakamchapa, na kukamata mikono yake. Wakiwa wamemkamata, polisi mmoja alinyanyua blauzi yake juu na kumgusagusa kwa njia isiyofaa alipokuwa akitafuta simu hiyo. Bibi alimzuia polisi huyo lakini hakukataa kukamatwa au kuwashambulia polisi hao.

Bibi, Vepa, na mwana wao

Kisha polisi waliichukua familia hiyo na kuwapeleka kwenye kituo cha polisi. Polisi walimtaka Vepa atie sahihi taarifa fulani waliyokuwa wameandaa. Vepa alikataa. Polisi walimpiga mara kadhaa wakati Bibi na mtoto wao walipokuwa kwenye chumba kingine. Lakini Vepa aliendelea kukataa. Bibi pia alikataa kutia sahihi taarifa hiyo na hivyo yeye pia alipigwa. Polisi walimweka kizuizini Bibi na mwana wake usiku huo na wakawaachilia siku iliyofuata. b Baada ya Bibi kupeleka malalamiko yake kwa wenye mamlaka, Vepa aliachiliwa Julai 11. Punde tu baada ya hapo, polisi wa mji wa Dashoguz walianza kuwapeleleza Bibi na mume wake.

Akamatwa, Awekwa Kizuizini, na Kufunguliwa Kesi Mahakamani

Bibi alikamatwa Agosti 6, akawekwa kizuizini Agosti 8, na kupandishwa kizimbani Agosti 18. Kesi hiyo ilipokuwa ikiendelea, Jaji Orazmuradov alionyesha upendeleo waziwazi. Mara kwa mara alimkatiza wakili wa Bibi alipokuwa akijaribu kumtetea. Polisi walipotoa ushahidi unaopingana, jaji alimzuia wakili wa Bibi asiwaulize maswali. Pia, jaji huyo alimkatiza Vepa kutoa ushahidi alipoanza kuelezea jinsi Bibi alivyotendewa vibaya na polisi na akakataa kusikiliza rekodi ya sauti ya matukio hayo. Jaji huyo alitoa uamuzi kwamba Bibi ana hatia na akamhukumu kifungo cha miaka minne gerezani.

Bibi anapaswa kukata rufani kabla ya Agosti 28, na hadi kufikia wakati huo ataendelea kuwa kizuizini katika gereza la DZD-7. Ikiwa rufani yake itakataliwa, atahamishiwa kwenye gereza la wahalifu, katika jangwa la Seydi. Hatanyimwa uhuru wake tu bali pia hatapata nafasi ya kumlea mtoto wake.

Ingawa Vepa hajashtakiwa rasmi, kuna uwezekano mkubwa sana kwamba atafunguliwa mashtaka ya uwongo na kuhukumiwa isivyo haki. Ikiwa hilo litatokea, mtoto wao hatakosa tu mama bali pia baba yake. Ukosefu huo mkubwa wa haki hauna msingi.

Ombi la Kutaka Haki Itendeke

Nchi ya Turkmenistan inajulikana kwa kuwatendea vibaya Mashahidi wa Yehova na kuwanyima haki zao za msingi za kibinadamu. Mashahidi wa Yehova ulimwenguni pote, pamoja na watu wengine wanaothamini haki ya kibinadamu ya kuheshimiwa na kuabudu kwa uhuru, wanatazamia serikali ya Turkmenistan itarekebisha makosa hayo.

a Adhabu ya kufanya fujo wakati wa kukamatwa na askari anayetekeleza sheria hufikia kifungo cha hadi miaka mitano gerezani.

b Mtoto wao aliachiliwa na kuchukuliwa na mtu wao wa ukoo asubuhi ya Julai 6; Bibi aliachiliwa baadaye siku hiyo.