Hamia kwenye habari

MEI 3, 2016
TURKMENISTAN

Polisi jijini Turkmenabad wawatesa wahudhuriaji wa ukumbusho wa kifo cha Kristo

Polisi jijini Turkmenabad wawatesa wahudhuriaji wa ukumbusho wa kifo cha Kristo

Machi 23, 2016, maofisa wa polisi walikusudia kuvuruga mkutano wa Mashahidi wa Yehova 20 uliofanywa katika nyumba ya mtu binafsi kwenye jengo moja la ghorofa lililopo jijini Turkmenabad, nchini Turkmenistan, kwa ajili ya kuadhimisha ukumbusho wa kifo cha Yesu. Polisi hao waliposhindwa kuingia ndani ya jengo hilo, waliendelea kulizingira. Wahudhuriaji wote hawakuweza kutoka ndani, hivyo walibaki hapo usiku kucha.

Siku iliyofuata, maofisa wanne wa polisi walivunja na kuingia ndani ya jengo hilo kupitia kibaraza cha ghorofani. Waliwatesa baadhi ya Mashahidi na kuwatendea kwa jeuri kiasi kwamba mwanamke mmoja mjamzito aliumia na kupelekwa hospitali. Wahudhuriaji wote walipelekwa kwenye kituo cha polisi, ambapo wanaume wawili ambao ni Mashahidi walipigwa. Machi 25, watu hao wote waliowekwa mahabusu waliruhusiwa kasoro mwanamume mmoja ambaye alitumikia kifungo cha siku 15. Aprili 19, wenye mamlaka waliwatoza faini Mashahidi saba na kila mmoja alilipa kiasi cha dola 143 hivi za Marekani. Walitozwa faini hizo bila hata kufikishwa mahakamani.