Hamia kwenye habari

Meli zilizokuja kwa ajili ya sherehe ya Armada, jijini Rouen, Ufaransa. Picha ndogo: Vigari vya machapisho vilivyowekwa ili kuwafikia watu katika sherehe hiyo

AGOSTI 18, 2023
UFARANSA

Mahubiri ya Hadharani Katika Sherehe ya Meli Jijini Rouen, Ufaransa

Mahubiri ya Hadharani Katika Sherehe ya Meli Jijini Rouen, Ufaransa

Baada ya kila miaka minne, tukio linaloitwa Armada hufanywa jijini Rouen, nchini Ufaransa. Meli kubwa zenye tanga kutoka sehemu mbalimbali ulimwenguni zinakuja kwa ajili ya tukio hilo. Mwaka huu tukio hilo lilifanywa kuanzia Juni 8 hadi 18. Lilihudhuriwa na zaidi ya wageni milioni sita kutoka nchi tofauti-tofauti. Mashahidi wa Yehova waliweka vigari vya machapisho katika sehemu 12 jijini humo kila siku. Zaidi ya ndugu na dada 600 walishiriki katika mahubiri hayo na walipata fursa ya kuzungumza na mamia ya watu.

Mpiga picha mmoja aliyestaafu alienda kwenye kigari na kuwaambia Mashahidi waliokuwepo kwamba amekutana na Mashahidi mara nyingi na kinachomvutia hasa ni fadhili na uchangamfu wao. Walizungumza kwa marefu kuhusu jinsi leo watu hawana upendo. Walizungumzia andiko la 2 Timotheo 3:1-5 na alikubali broshua Furahia Maisha Milele! Aliwapa namba yake ya simu na kusema kwamba anatazamia kwa hamu kuzungumza tena na Mashahidi.

Pindi nyingine, mwanamke mmoja alikuja kwenye kigari na kuuliza: “Yesu alikufa, akafufuka. Mbona wapendwa wetu bado hawajafufuka? Babu na nyanya yangu walikufa na ninatamani sana kuwaona tena.” Ili kumfariji, dada yetu alimwonyesha video yenye kichwa Faraja kwa Wanaoomboleza. Baada ya mazungumzo hayo alipokea broshua na akakubali kujifunza Biblia.

Tunafurahi pamoja na ndugu na dada zetu nchini Ufaransa ambao walitumia muda na nguvu zao ‘ili kuishiriki habari njema pamoja na wengine.’​—1 Wakorintho 9:23.