DESEMBA 12, 2012
UFARANSA
Ufaransa Yarudisha Pesa Ilizochukua Kutoka kwa Mashahidi wa Yehova Kinyume cha Sheria
Desemba 11, 2012, baada ya kesi iliyoendelea kwa miaka 15, serikali ya Ufaransa iliwalipa Mashahidi wa Yehova euro 6,373,987.31 (dola 8,294,320).
Mnamo 1998, serikali ilisema kwamba michango ya kidini inayotolewa na Mashahidi wa Yehova, kutia ndani michango iliyokuwa imetolewa miaka ya mapema, inapaswa kutozwa kodi ya asilimia 60 na, katika mwaka wa 2003, serikali ilidai ilipwe sehemu ya pesa hizo. Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu ilisema kwamba Ufaransa ina hatia ya kuingilia uhuru wa kidini wa Mashahidi wa Yehova kwa kuwatoza kodi hiyo isiyo halali, jambo ambalo, ikiwa lingetekelezwa, lingefanya Mashahidi wa Yehova wauze ofisi zao zote na kuzuia kazi yao ya kuwafundisha watu Biblia. Kwa kuwa Mahakama hiyo iliamua kwamba kodi hiyo haikuwa halali, serikali ya Ufaransa imeanza kutii uamuzi wa Mahakama hiyo kwa kurudisha pesa ilizochukua, pamoja na riba, na pia kulipia gharama ambazo Mashahidi walipata katika kesi hiyo.
Wanahabari Wanaweza Kuwasiliana na:
J. R. Brown, Ofisi ya Habari za Umma, simu +1 718 560 5000
Ufaransa: Guy Canonici, simu +33 2 32 25 55 55