JANUARI 7, 2019
UGIRIKI
Kukumbuka Pambano la Miaka 50 la Kutafuta Uhuru wa Kuhubiri
Miaka 80 iliyopita, Minos Kokkinakis alishuka kutoka kwenye mashua ya gereza katika kisiwa cha Ugiriki cha Amorgós kilichoko kwenye Bahari ya Aegea, ambako angetumikia akiwa uhamishoni kwa miezi 13. Bila kushtakiwa, mahakama ya Ugiriki ilimhukumu Ndugu Kokkinakis kwa kuvunja sheria mpya iliyokataza kutafuta washiriki wapya wa dini. Alikuwa wa kwanza kukamatwa kati ya Mashahidi wa Yehova 19,147 walioshtakiwa kuanzia mwaka wa 1938 hadi 1992 kwa kuvunja sheria iliyowekwa na dikteta Mgiriki aliyeitwa Ioannis Metaxas. Katika miaka hiyo, mamia ya Mashahidi Wagiriki waliendelea kuhubiri habari njema licha ya hatari ya kutendewa kwa jeuri, kukamatwa, na kufungwa gerezani.
Alipokuwa na umri wa miaka 30, Ndugu Kokkinakis alianza pambano la kisheria la miaka 50 la kutafuta uhuru wa kuwahubiria wengine kuhusu imani yake. Alikamatwa mara zaidi ya 60, alifungwa gerezani na kwenye visiwa vilivyotumiwa kama magereza kwa miaka zaidi ya sita, ambako yeye na Mashahidi wengine walivumilia hali mbaya sana. Alipokuwa na umri wa miaka 77, alijaribu bila mafanikio kupinga kisheria kukamatwa mara ya mwisho. Kesi yake hata ilifika kwenye Mahakama Kuu ya Ugiriki. Baada ya hapo, Ndugu Kokkinakis alipeleka ombi lake Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu (ECHR), akisema kwamba nchi ya Ugiriki ilikuwa imemnyima haki yake ya kidini. Mwaka wa 1993, Minos Kokkinakis ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka 84 alipata ushindi wa pambano la kutafuta haki yake ya kisheria, hiyo ikiwa mara ya kwanza kwa ECHR kusema kwamba nchi imekiuka uhuru wa kidini. a Mwaka wa 2018 ulikuwa mwaka wa 25 tangu uamuzi huo wa kihistoria utolewe. Kulingana na profesa mmoja wa sheria ya kimataifa, kesi ya Kokkinakis “huenda ndiyo hukumu inayotajwa mara nyingi zaidi katika Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu kuhusiana na uhuru wa kidini au wa imani.”
Uamuzi wa Kokkinakis bado unatumika kisheria katika visa vingine katika enzi ambayo serikali zenye nguvu kama Urusi, zinajaribu kuwanyima ndugu zetu wengi haki ya kuabudu bila kuingiliwa.
Imani ya Ndugu Kokkinakis na ustahimilivu katika huduma ni mfano mzuri sana kwa ndugu na dada zetu wanaokabili upinzani dhidi ya kazi yao ya kuhubiri. Utimilifu wake ulitokeza ushahidi mkubwa ambao bado unakumbukwa hadi leo.—Waroma 1:8.
a Minos Kokkinakis alikufa Januari 1999.