Hamia kwenye habari

Juu: Jengo la Betheli lililokuwa Amsterdam mwaka 1964. Chini: Ndugu na dada wakifanya kazi ndani ya ofisi za Betheli katika miaka ya 1950 na 1960

OKTOBA 7, 2022
UHOLANZI

Uholanzi Imetimiza Karne Nzima Yenye Majaribu na Ushindi

Uholanzi Imetimiza Karne Nzima Yenye Majaribu na Ushindi

Mwaka huu wa 2022, ni mwaka wa 100 tangu ofisi ya tawi ilipoanzishwa katika Amsterdam, mji mkuu wa Uholanzi. Katika kipindi hicho cha miaka 100, ndugu na dada zetu nchini humo wameonyesha imani yenye nguvu na pia ujasiri.

Kweli ilifika Uholanzi mwanzoni mwa mwaka wa 1900, mwanamume mmoja kijana aliyeitwa Heinrich Brinkhoff alipoanza kusoma machapisho ya Watch Tower Society na International Bible Students Association. Punde si punde, akaanza kuzungumza na wengine kuhusu mambo aliyojifunza. Mbegu za kweli alizopanda ziliendelea kukua. Mwaka 1920, Ndugu Joseph F. Rutherford alitembelea Ulaya na kuanzisha ofisi ya tawi nchini Uswisi. Mwanzoni, ofisi hiyo ilisimamia kazi katika Uholanzi pia. Mwaka 1921, Ndugu Rutherford alimteua Ndugu Adriaan Block ili asimamie kazi nchini Uholanzi. Mwaka 1922, ofisi ya tawi ilifunguliwa jijini Amsterdam.

Baada ya kuwa na ofisi ya tawi, kazi ya kuhubiri ilifanywa kwa utaratibu zaidi. Idadi ya watumishi wa Yehova iliendelea kuongezeka. Muda mfupi kabla ya Vita vya Pili vya Ulimwengu, kulikuwa na angalau wahubiri 500 wanaotenda nchini Uholanzi.

Vita hivyo vilipoanza, Uholanzi ilivamiwa na Wanazi. Wanazi hao waliwatesa sana Mashahidi wa Yehova na pia makundi mengine ya watu. Katika kipindi hicho, Mashahidi 300 kutoka Uholanzi walifukuzwa nchini humo na wengi wao wakapelekwa kwenye kambi za mateso. Ndugu zetu 130 hivi walikufa kwa sababu ya magonjwa au hali nyingine ngumu. Licha ya mateso yaliyoendelea nchini humo, idadi ya Mashahidi iliongezeka. Kulikuwa na Mashahidi 3,125 vita vilipoisha katika mwaka wa 1945.

Kwa kusikitisha, majaribu yaliendelea hata baada ya vita kwisha. Kanisa Katoliki liliwapinga sana Mashahidi, hasa katika sehemu ya kusini ya nchi hiyo. Mfano mmoja ni jambo lililotukia mwaka wa 1952. Kanisa hilo lilijaribu kuzuia kusanyiko kufanywa jijini Venlo. Upinzani huo uliwachochea wamiliki wa mahali ambapo kusanyiko lingefanywa wafute mkataba wao na Mashahidi wa Yehova. Mashahidi hao hawakuvunjika moyo, waliweka hema kwenye uwanja uliokuwa wazi, na wakafanya kusanyiko katika eneo hilo.

Upinzani haukuisha. Kundi kubwa la watu zaidi ya 1,000 lilienda kwenye eneo la kusanyiko ili kuvuruga programu. Hata maofisa wa polisi walivamia eneo hilo la kusanyiko na kuwakamata baadhi ya ndugu zetu katika kipindi cha Jumapili mchana.

Ofisi ya tawi iliyo Emmen leo

Jitihada zote za wapinzani hao hazikufanikiwa. Akina ndugu waliosimamia walifuata mwongozo wa ofisi ya tawi na wakafaulu kuendelea na kusanyiko hilo.

Yehova aliendelea kubariki bidii ya ndugu zetu nchini humo. Mwaka 1983, ofisi ya tawi ya Uholanzi ilihamishiwa kwenye majengo mapya katika mji wa Emmen. Kwa sasa, yaani, mwaka wa 2022, kuna Mashahidi karibu 30,000 nchini Uholanzi.

Historia ya Mashahidi wa Yehova nchini Uholanzi inathibitisha kwamba Yehova “hatawatupa wala kuwaacha” watu wake.​—Kumbukumbu la Torati 31:6.