SEPTEMBA 5, 2017
UINGEREZA
Ofisi Mpya ya Tawi Nchini Uingereza Imepata Tuzo Bora ya BREEAM kwa Muundo Mzuri
LONDON—Mashahidi wa Yehova wanajenga majengo mapya ya kusimamia kazi nchini Uingereza na muundo wa ujenzi umepata tuzo bora zaidi ulimwenguni ya viwango vya ujenzi, BREEAM (Building Research Establishment Environmental Assessment Method). Majengo hayo ya Mashahidi, yanajengwa eneo lililopo kilomita 70 mashariki ya London, huko Chelmsford, Essex, na ni mradi wa pili kuwa na viwango vya juu vya ujenzi kulingana na BREEAM.
BREEAM, iliyoanzishwa na kituo kinachojulikana cha uchunguzi wa ujenzi BRE (Building Research Establishment), inapima ubora wa miradi ya ujenzi, miundo-mbinu, na majengo katika vikundi kadhaa: nishati, ubora wa majengo, ubunifu, matumizi ya ardhi, vifaa, usimamizi, uchafuzi, usafirishaji, kuondoa taka, na mfumo wa maji. Kisha miradi hiyo inawekwa katika vitengo kadhaa Sawa, Nzuri, Nzuri Sana, Bora, au Bora Sana. Ili wakubali michoro ya ofisi mpya ya Mashahidi, Manispaa ya Jiji la Chelmsford iliwawekea matakwa ya muundo bora, mojawapo ikiwa kupata kiwango cha Nzuri Sana cha ubora kulingana na BREEAM. Neil Jordan, ofisa wa mipango wa Manispaa ya Jiji la Chelmsford katika kitengo kinachohusiana na ujenzi bora kwa kuzingatia mazingira na udumishaji, anasema hivi kuhusu mradi wa Mashahidi: “Tunafurahi kwamba Mashahidi wa Yehova wametimiza kikamili matakwa ya mradi huo, hata wamepita viwango vilivyotarajiwa na manispaa ya jiji.” Anasema kwamba mradi huo “sasa unaweza kusemwa kuwa jambo la kujivunia jijini mwetu, na linaongoza katika kufikia kiwango bora zaidi cha mazingira.”
Zaidi ya kupata tuzo bora zaidi, mradi huo pia ulitambuliwa kwa kutunza mazingira. Mashahidi walipunguza gesi ya kaboni kwa tani 2,480 kwa kuwapa wafanyakazi makao kwenye eneo la ujenzi na kuwasafirisha wakitumia mabasi madogo na magari mengine yasiyochafua sana hewa. Hilo lilifanya Mashahidi wapate “tuzo ya ubunifu” kutoka kwa BREEAM, tuzo kama hiyo haijawahi kutolewa. Bw. Jordan anaeleza kwamba mradi “ulichangia katika kupata njia mpya za kupunguza gesi ya kaboni, na kufaulu kupata tuzo ya BREEAM katika mambo ambayo hayajawahi kutuzwa katika masuala ya mazingira.”
Bw. Pallab Chatterjee, mkaguzi wa BREEAM, anasema hivi kuhusu kufanya kazi na Mashahidi na uhusiano wao na jamii kwa ujumla: “Nilifurahia mtazamo mzuri wa kirafiki uliokuwepo katika eneo la ujenzi, jambo ambalo si la kawaida hata kidogo. Mashahidi walijaribu kuhusisha mawazo mengi ya BREEAM iwezekanavyo katika muundo wa ujenzi wao. Walikazia fikira muundo ambao ungeongeza thamani ya ujenzi bali si kupata tuzo la BREEAM tu. Nilipendezwa na mazungumzo marefu yaliyofanywa kati yao na jamii jirani na watu watakaoishi humo. Ni mradi niliofurahia zaidi kuufanyia kazi.”
Andrew Schofield, msemaji wa Mashahidi wa Yehova nchini Uingereza alisema hivi: “Kwa miaka 60 hivi, ofisi zetu zimekuwa jijini London. Hata hivyo, kwa sababu ya uhitaji ulioongezeka wa machapisho na vifaa vya Biblia, tulihitaji eneo kubwa zaidi. Aprili 2015 tulianza kazi ya kutayarisha eneo la ekari 34 na ujenzi unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka wa 2019.”
Wanahabari Wanaweza Kuwasiliana na:
David A. Semonian, Ofisi ya Habari za Umma, simu +1-845-524-3000
Uingereza: Andrew Schofield, simu +44-20-8906-2211