Hamia kwenye habari

Balozi Thomas Pröpstl akimpa Dada Simone Arnold-Liebster tuzo kutoka serikali ya Ujerumani

JANUARI 24, 2024
UJERUMANI

Ujerumani Yampa Simone Arnold-Liebster Tuzo kwa Kazi Anayofanya ili Kuelimisha Vijana

Ujerumani Yampa Simone Arnold-Liebster Tuzo kwa Kazi Anayofanya ili Kuelimisha Vijana

Desemba 15, 2023, Dada Simone Arnold-Liebster alitunukiwa tuzo iliyotolewa na Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani. Hiyo ni tuzo ya heshima sana ambayo mtu hutunukiwa kwa sababu ya kujitoa kwa bidii katika jamii. Simone alipewa tuzo hiyo na Balozi Mkuu wa Ujerumani, Thomas Pröpstl kwenye sherehe iliyofanywa Chambéry, Ufaransa. Sasa Simone ana umri wa miaka 93. Alipongezwa kwa sababu ya jitihada anazofanya ili kuwasaidia watu wasisahau jinsi serikali ya Wanazi ilivyowatendea kwa ukatili na chuki wale waliokataa kuiunga mkono.

Kufikia sasa, Simone amezungumza na watu katika nchi 25. Karibu watu 65,000 wamehudhuria mikutano yake, kutia ndani wanafunzi wengi na walimu. Licha ya kwamba umri wake umesonga, anaendelea kufanya mikutano hiyo kupitia video mtandaoni ambapo anajibu maswali ya vijana na kuwasimulia mambo aliyojifunza alipokuwa na umri kama wao. Mwanafunzi mmoja aliyehudhuria mkutano wake aliandika hivi: “Baada ya kusikiliza simulizi la maisha la Simone, nimejifunza kwamba tunaweza kuwa imara tunapokuwa na imani yenye nguvu.”

Simone Arnold-Liebster akizungumza na kikundi cha wanafunzi waliokuwa Colorado, nchini Marekani, kupitia video mtandaoni

Balozi Thomas Pröpstl alipompa Simone tuzo alisema: “Ni ajabu kwamba umeweza kupata nguvu kutokana na mateso uliyopitia mwenyewe. Sikuzote umesimulia mambo hayo kwa unyoofu na kwa fadhili huku ukiwa na uhakika kwamba kutakuwa na amani wakati ujao. Kwa sababu hiyo, ninakuheshimu sana.”

Simone na familia yake waliteswa sana chini ya utawala wa Wanazi kama tu maelfu ya Mashahidi wengine wa Yehova. Alipokuwa na umri wa miaka 12, alichukuliwa na Wanazi na kupelekwa kwenye shule ya kuwarekebisha watoto ya Von Wessenberg iliyo Konstanz nchini Ujerumani, kwa kusudi la kumlazimisha akubali na kuunga mkono serikali hiyo. Kwa kuwa alikataa katakata kufanya hivyo, alidhalilishwa, alipewa chakula kidogo sana, alifanyishwa kazi ya lazima, na alikatazwa kuzungumza kwa miaka miwili hivi. Simone anapokumbuka mambo hayo anasema: “Yehova amenitegemeza; nilidumisha utimilifu wangu.”

Tunatiwa moyo kujua kuhusu rekodi ya utimilifu ambayo Simone alidumisha kwa uaminifu kadiri anavyoendelea kumtukuza Baba yetu, Yehova Mungu.​—Mathayo 5:16.