Hamia kwenye habari

JULAI 16, 2015
UJERUMANI

Maofisa Wawapatia Tuzo Baba na Mtoto kwa Kusaidia Kuwaokoa Wanaume Watatu Kutoka Gari Lililowaka Moto

Maofisa Wawapatia Tuzo Baba na Mtoto kwa Kusaidia Kuwaokoa Wanaume Watatu Kutoka Gari Lililowaka Moto

Jorim, Christiane, na Andreas Bonk. Andreas alikuwa amelazwa hospitali wakati wa sherehe hizo kutokana na tukio lingine lisilohusiana na hilo.

SELTERS, Ujerumani—Mnamo Aprili 16, 2015, Shahidi wa Yehova aitwaye Andreas Bonk, pamoja na mwana wake Jorim, walikuwa miongoni mwa watu waliopewa tuzo kwa sababu ya kuwaokoa wanaume watatu waliokuwa ndani ya gari lililopata aksidenti na kuwaka moto. Zawadi hizo zilitolewa katika sherehe iliyohudhuriwa na waziri wa mambo ya ndani wa Serikali ya Jimbo la Baden-Württemberg, lililopo kusini-magharibi mwa Ujerumani, pamoja na meya wawili kutoka Obersulm na Waiblingen, eneo analoishi Bonk na familia yake. Waziri wa Mambo ya Ndani Reinhold Gall (picha ya juu, wa tatu kutoka kulia) alimtunuku Andreas Bonk Nishani ya Kuokoa Maisha inayotolewa na Serikali ya Jimbo la Baden-Württemberg (Lebensrettungsmedaille des Landes Baden-Württemberg). Kwa kuwa Bw. Bonk alikuwa amelazwa hospitali wakati wa sherehe hizo kutokana na tukio lingine lisilohusiana na hilo, mke wake Christiane (picha ya juu, katikati), alipokea nishani hiyo. Katika sherehe hiyo, meya wa Obersulm, Tilman Schmidt (picha ya juu, kushoto kabisa), alimtunuku Jorim Bonk (picha ya juu, katikati) Cheti cha Heshima (Ehrungsurkunde).

Mei 11, 2014, Andreas and Jorim Bonk walikuwa wakisafiri kwenye barabara kuu kuelekea katika mkutano mkubwa wa elimu ya Biblia uliotayarishwa na Mashahidi wa Yehova ambapo Andreas alipangiwa kutoa hotuba inayotegemea Biblia. Wakiwa njiani, walikuta gari lililopata aksidenti. Wanajeshi wanne wa Marekani walishindwa kutoka ndani ya gari lililokuwa limeanguka upande na kuwaka moto. Familia ya Bonk na watu wengine wawili walianza kuwasaidia. Andreas alihatarisha uhai wake ili kuwasaidia abiria hao watoke ndani ya gari lililowaka moto mpaka polisi, idara ya zima moto, na gari la wagonjwa lilipofika. Inasikitisha kwamba mwanajeshi mmoja alikufa. Likizungumzia habari hiyo, gazeti Sulmtaler Woche lilimnukuu Waziri Gall akiwaeleza waokoaji hao, “Mmetenda kwa ujasiri, ushujaa, na bila ubinafsi.” Meya Schmidt aliongezea, “Watu wote wa Obersulm wanawapongeza sana.”

Picha ya eneo la tukio.

Andreas Bonk anaeleza jambo lililomchochea kutenda kwa ujasiri: “Nilisimama ili kutoa msaada katika eneo la aksidenti kwa sababu ninawajali wanadamu wenzangu. Mimi ninaona kwamba uhai wowote ni wenye thamani sana. . . . Ikiwa mimi au ndugu zangu watapatwa na hali kama hiyo, ninatumaini kwamba watu wengine watahisi hivyo pia na kuwa tayari kwa ujasiri kusaidia.” Jorim aliongezea hivi, “Ni muhimu sana kutopuuza watu wenye uhitaji.”

Sherehe ya kutoa tuzo hizo ilifanyika kwenye Ukumbi wa Mji wa Obersulm. Gazeti habari la Ujerumani liitwalo STIMME.de liliandika habari kuhusu sherehe hiyo na kumnukuu meya wa Waiblingen, Andreas Hesky (picha ya juu, wa pili kutoka kulia), akisema: “Mnapaswa kujivunia jambo mlilofanya. Mji wa Waiblingen unajivunia kuwa na raia kama ninyi. Ninyi ni mfano mzuri kwa jamii yetu.”

Wanahabari wanaweza kuwasiliana na: J. R. Brown, Ofisi ya Habari za Umma, simu. +1 718 560 5000

Ujerumani: Wolfram Slupina, simu. +49 6483 41 3110