Hamia kwenye habari

Ndugu Oleksandr Tretiak

DESEMBA 28, 2020
UKRAINIA

ECHR Yatoa Uamuzi Unaomtetea Ndugu Oleksandr Tretiak, Aliyepigwa kwa Sababu ya Imani Yake

ECHR Yatoa Uamuzi Unaomtetea Ndugu Oleksandr Tretiak, Aliyepigwa kwa Sababu ya Imani Yake

Alhamisi, Desemba 17, 2020, Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu (ECHR) ilitoa uamuzi unaomtetea Ndugu Oleksandr Tretiak katika kesi ya Tretiak v. Ukraine. Ndugu Tretiak alipigwa vibaya sana na watu watatu Novemba 26, 2013, alipokuwa akielekea nyumbani baada ya kushiriki katika kazi ya kuhubiri. ECHR ilitoa uamuzi kwamba wenye mamlaka nchini Ukrainia hawakupeleleza vya kutosha uhalifu huo. Mahakama iliamuru kuwa fidia ya kiasi cha euro 7,500 (dola 9,000 za Marekani) inapaswa kulipwa.

Ndugu Tretiak alipigwa vibaya sana hivi kwamba alilazwa mwezi mmoja hospitalini. Polisi hawakufanya uchunguzi eneo ambalo uhalifu huo ulitendeka mpaka baada ya miezi mitatu kupita baada ya shambulio hilo. Walikataa pia kutoa tamko kuwa shambulio hilo lilichochewa na chuki ya kidini na walikataa kukiri kwamba Ndugu Tretiak alikuwa ameumizwa vibaya sana. Baadaye, polisi walipunguza kiwango cha mashtaka dhidi ya washambuliaji kufikia uhalifu mdogo. Kwa kuongezea, walimshtaki mshambuliaji mmoja tu kati ya watatu—baada ya mtu huyo kuondoka nchini humo. Washambuliaji wengine wawili, mmoja wao akiwa polisi, walionwa kuwa kama mashahidi katika kesi hiyo. Hakuna yeyote aliyeadhibiwa. Hali hizo na nyingine za ukosefu wa haki zilimchochea Ndugu Tretiak kupeleka kesi yake ECHR mwaka wa 2015.

Katika uamuzi wake, ECHR ilimalizia kwa kusema “Mamlaka za [Ukrainia] zilishindwa kufanya upelelezi kikamili dhidi ya mashtaka ya kutendewa isivyo haki yaliyoletwa na mlalamikaji,” kitendo kinachokiuka Mkataba wa Ulaya wa Haki za Kibinadamu.

Ni matumaini yetu kwamba uamuzi huu utasaidia kulinda uhuru wa ibada wa ndugu na dada zetu katika Ukrainia na nchi nyingine. Zaidi ya yote, tunamshukuru Yehova, anayetutendea kwa haki.—Maombolezo 3:59.