APRILI 1, 2022
UKRAINIA
RIPOTI YA 5 | Upendo wa Kindugu Unaendelea Kuonyeshwa Licha ya Mashambulizi Nchini Ukrainia
Kwa kusikitisha, kufikia Machi 29, 2022, ndugu na dada wengine saba katika jiji la Mariupol wamekufa. Kwa ujumla, ndugu na dada 17 wamekufa kufikia sasa nchini Ukrainia.
Halmashauri za Kutoa Msaada (DRC) nchini Ukrainia zinafanya kazi nyingi ili kuandaa msaada, hata ikiwa wanalazimika kuhatarisha uhai wao wenyewe.
Kwa mfano, ndugu wanaofanya kazi katika halmashauri hizo wamefaulu kupeleka chakula, dawa, na mahitaji mengine katika miji iliyoathiriwa vibaya, kama vile Kharkiv, Kramatorsk, na Mariupol. Mshiriki mmoja wa DRC huwa anasafiri zaidi ya kilomita 500 kila siku, akipita vituo vingi sana vya ukaguzi wa kijeshi, ili kufikisha chakula na dawa kwa wahubiri 2,700 hivi.
Pia, halmashauri hizo hupanga usafiri wa kuwaokoa ndugu na dada zetu kutoka katika maeneo ya vita. Ndugu mmoja wa DRC ya Chernihiv anasema hivi: “Jeshi lilipoanza kulipua makao ya watu, ilikuwa wazi kwamba ni hatari sana kuendelea kukaa katika jiji hili. Kwa kuwa hakukuwa na umeme na Intaneti haikuwa ikafanya kazi, wazee walienda upesi kotekote jijini huku makombora yakilipuliwa na kuwajulisha wahubiri waliokuwa wakijificha katika vyumba vya chini ya ardhi kwamba usafiri unapatikana wa kuwawezesha kuondoka jijini.”
Mmiliki wa biashara ya usafiri alikubali tutumie mabasi yake, naye alienda safari tisa ili kuwaokoa ndugu na dada 254 kutoka Chernihiv. Pindi moja hata alirekebisha barabara akitumia mashine zenye nguvu ili basi lake liweze kupita. Ndugu zetu walishukuru sana kwa msaada huo.
Tunahuzunika pamoja na wale ambao wamewapoteza wapendwa wao wakati wa vita vinavyoendelea. Sote tunatazamia wakati ambapo tumaini linalotajwa katika Neno la Mungu, Biblia litatimia, wakati ambapo kifo na maombolezo hayatakuwepo tena.—Ufunuo 21:3, 4.
Kufikia Machi 29, 2022, hizi ndizo takwimu zilizotufikia kutoka Ukrainia. Takwimu hizo zinategemea ripoti za uhakika tulizopata kutoka kwa ndugu walio katika maeneo hayo. Hata hivyo, huenda idadi halisi ikawa kubwa zaidi kwa sababu ni vigumu kudumisha mawasiliano mazuri katika maeneo yote nchini.
Athari Ambazo Ndugu na Dada Zetu Wamepata
Wahubiri 17 wamekufa
Wahubiri 35 wamejeruhiwa
Wahubiri 36,313 wameacha makao yao na kwenda sehemu zilizo salama zaidi nchini.
Nyumba 114 zimeharibiwa kabisa
Nyumba 144 zimepata uharibifu mkubwa
Nyumba 612 zimepata uharibifu mdogo
Jumba 1 la Ufalme limeharibiwa kabisa
Majumba 7 ya Ufalme yamepata uharibifu mkubwa
Majumba 23 ya Ufalme yamepata uharibifu mdogo
Jitihada za Kutoa Msaada
Halmashauri 27 za kutoa msaada zinashughulikia hali nchini Ukrainia
Wahubiri 37,739 wamesaidiwa moja kwa moja na halmashauri hizo kupata makao salama zaidi
Wahubiri 16,175 wamekimbilia nchi nyingine na wanasaidiwa na waamini wenzetu