OKTOBA 31, 2019
UKRAINIA
Uamuzi wa Mahakama ya ECHR Wafungua Njia ya Kujenga Jumba la Ufalme Nchini Ukrainia
Septemba 3, 2019, Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu (ECHR) ilitoa uamuzi uliowaunga mkono Mashahidi wa Yehova katika jiji la Kryvyi Rih, Ukrainia. Mahakama hiyo ilitoa uamuzi kwamba halmashauri ya jiji la Kryvyi Rih ina hatia ya kukataa kimakusudi kuwapa akina ndugu kibali cha kujenga Jumba la Ufalme.
Mahakama hiyo iliamua kwamba jiji hilo linapaswa kulipa makutaniko mawili yanayomiliki eneo hilo dola $7,768 hivi za Marekani ambazo ni gharama za kuendesha kesi na kwa kukiuka sheria za kimataifa—Kifungu cha 9 (kinacholinda uhuru wa kufikiri, dhamiri, na kidini) na Kifungu cha 1 cha Mkataba Na. 1 (kinacholinda haki ya kumiliki mali) katika Mkataba wa Ulaya Kuhusu Haki za Kibinadamu. Serikali ya Ukrainia imepewa miezi mitatu ya kupinga uamuzi huo na kukata rufaa kwenye baraza kuu la ECHR.
Zaidi ya miaka 15 imepita tangu makutaniko hayo mawili huko Kryvyi Rih yalipotuma maombi ya kwanza ya kujenga Jumba la Ufalme. Agosti 9, 2004, walinunua jengo la makazi kwenye kiwanja kinachosimamiwa na jiji hilo na wakaomba kukodi kiwanja hicho kwa miaka mitano ili kujenga Jumba la Ufalme. Halmashauri ya jiji ilitoa kibali cha kwanza Septemba 28, 2005. Isitoshe, halmashauri ya jiji iliwataarifu ndugu zetu kwamba pendekezo la mradi wao linapaswa kuidhinishwa na maofisa fulani wa serikali kabla ya kupata kibali cha mwisho wanachohitaji ili kuanza ujenzi.
Mipango hiyo ilifuatiliwa na kuidhinishwa na maofisa wa serikali wanaohusika, kisha Agosti 23, 2006 ikawasilishwa kwa halmashauri ya jiji ili kupata kibali cha mwisho. Ingawa kulingana na sheria halmashauri ya jiji inapaswa kutoa uamuzi ndani ya mwezi mmoja, haikujibu maombi ya ndugu zetu. Hata baada ya mahakama katika eneo hilo kuthibitisha kwamba halmashauri ya jiji ilitenda kinyume na sheria, bado halmashauri hiyo ilikataa kutoa kibali cha mwisho. Hata baada ya kukata rufaa mara kadhaa akina ndugu hawakufanikiwa, basi Aprili 13, 2010, waliamua kupeleka malalamiko yao kwenye mahakama ya ECHR.
Tunafurahi kwamba mahakama ya ECHR ilitoa uamuzi uliowaunga mkono ndugu zetu huko Kryvyi Rih. Tunasali kwamba uamuzi wa ECHR utaweka msingi wa kisheria wa kuwasaidia ndugu zetu kujenga majengo kwa ajili ya kumwabudu Yehova katika nchi ambazo wananyimwa haki hiyo.—Zaburi 118:5-9.