Hamia kwenye habari

Waabudu wenzetu huko Kharkiv, Ukrainia, wakiwa wamejificha makombora yalipokuwa yakilipuliwa

MACHI 3, 2022
UKRAINIA

Upendo wa Kindugu Unaendelea Kuonyeshwa Licha ya Mashambulizi Nchini Ukrainia

Upendo wa Kindugu Unaendelea Kuonyeshwa Licha ya Mashambulizi Nchini Ukrainia

Februari 24, 2022, Urusi ilishambulia Ukrainia. Kuna zaidi ya Mashahidi 129,000 wa Yehova pamoja na watoto wao nchini Ukrainia. Ofisi ya tawi imepanga Halmashauri 27 za Kutoa Msaada (DRC) ili kuwaandalia ndugu zetu msaada wa kibinadamu. Mbali na hilo, ili kuonyesha upendo wao wa Kikristo, ndugu na dada wanafanya jitihada za kuandaa msaada halisi na faraja miongoni mwao na kwa jirani zao wakati wa mashambulizi hayo.

Ingawa ndugu na dada wengi bado wako nchini, baadhi wamefanya uamuzi wa kibinafsi wa kukimbia. Waliokuwa wakikimbia walikuta mistari mirefu, ambayo mingine ilikuwa na urefu wa kilomita 30, na wakasubiri kwa siku mbili au tatu ili kuvuka mpaka. Wahubiri wa maeneo hayo waliwatafuta waabudu wenzao waliokuwa wamepanga mstari na kuwaandalia vyakula na msaada halisi. Ndugu na dada hao walipovuka mipaka na kuingia nchi jirani, walipokewa na Mashahidi waliokuwa wamebeba ishara ya jw.org wakiwa tayari kuwafariji na kuwapa msaada unaohitajika.

Dada zetu nchini Poland (kushoto) na Slovakia (kulia) wakisubiri ili kuwaandalia msaada waabudu wenzao wanaokimbia kutoka Ukrainia

Athari Ambazo Ndugu na Dada Zetu Wamepata

  • Ndugu Petro Mozul, mtumishi wa huduma ambaye ni kiziwi jijini Kharkiv, alikufa kutokana na makombora

    Kwa kusikitisha, Machi 1, 2022, ndugu 1 kiziwi katika eneo la Kharkiv alikufa na mke wake akajeruhiwa vibaya kutokana na makombora yaliyorushwa

  • Dada wengine 3 walijeruhiwa

  • Zaidi ya wahubiri 5,000 wamekimbia kutoka nyumbani kwao

  • Nyumba 2 zilibomolewa

  • Nyumba 3 zilipata uharibifu mkubwa

  • Nyumba 35 zilipata uharibifu mdogo

  • Majumba 2 ya Ufalme yaliharibiwa

  • Wahubiri wengi wamelazimika kuishi bila umeme, mifumo ya kupasha nyumba joto, huduma za simu, na maji

Jitihada za Kutoa Msaada

  • Halmashauri 27 za Kutoa Msaada zimewekwa rasmi nchini Ukrainia

  • Wahubiri 867 wamesaidiwa na halmashauri hizo kupata mahali pa kulala katika maeneo salama zaidi

  • Halmashauri hizo zinafanya kazi ili kuandaa mahitaji muhimu kama vile chakula na maji

Tarakimu zilizotajwa juu ni ripoti za awali.

Tunasali kwamba ndugu na dada zetu waendelee kutenda kwa hekima na uelewaji wanapovumilia hali hizo zisizoeleweka na mikazo inayotokea, huku wakiendelea kuonyesha upendo wa kindugu.​—Methali 9:10; 1 Wathesalonike 4:9.