Hamia kwenye habari

JUNI 8, 2015
UKRAINIA

Mahakama za Ukrainia Zatambua Haki ya Kutojiunga na Jeshi Wakati wa Vita

Mahakama za Ukrainia Zatambua Haki ya Kutojiunga na Jeshi Wakati wa Vita

Kwa sababu ya machafuko na vita vilivyozuka katika maeneo ya mashariki ya Ukrainia mwaka wa 2014, rais wa Ukrainia aliamuru watu wengi zaidi wajiandikishe jeshini. Vitaliy Shalaiko, aliyekuwa mwanajeshi kabla ya kuwa Shahidi wa Yehova, aliamriwa aende kujiandikisha. Bw. Shalaiko, alimweleza msimamizi wa idara ya chakula jeshini kwamba hatajiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri na akaeleza kuwa yuko tayari kufanya utumishi mwingine wa badala.

Ofisi ya jeshi ilikataa maelezo ya Bw. Shalaiko na kumfungulia mashtaka ya kukataa utumishi wa jeshi wakati wa vita. Katika vita vinavyoendelea, hii ni mara ya kwanza mtu kushtakiwa nchini Ukrainia kwa kukataa utumishi wa kijeshi kwa msingi wa imani ya kidini wakati nchi ikiwa vitani.

Kwa kuwa alikuwa mwanajeshi, Bw. Shalaiko anaelewa nia ya serikali ya kulinda taifa na raia zake. Hata hivyo, kuhusu wito huo wa utumishi wa jeshi, Bw. Shalaiko alifuata kanuni ya Biblia ya mlipeni “Kaisari vitu vya Kaisari, lakini Mungu vitu vya Mungu.” a Kwa kuwa yeye ni mhudumu Mkristo, anaheshimu uhai wa mwanadamu na anawapenda watu wote. b

Shtaka: Je Utumishi wa Badala Ni Kukataa Kimakusudi Kujiunga na Jeshi?

Novemba 13, 2014, Mahakama ya Wilaya ya Novomoskovsk katika eneo la Dnipropetrovsk ilisikiliza kesi ya Bw. Shalaiko aliyeshtakiwa kukataa utumishi wa kijeshi wakati wa vita. Mahakama ilitambua kuwa hakukataa kufika mbele ya wenye mamlaka, bali alitii na kufika katika ofisi za jeshi kama alivyoamriwa. Mahakama iliamua kwamba Bw. Shalaiko “ana haki ya kuchagua aina nyingine ya utumishi ulio wa badala, hata wakati wa vita, kwa sababu ni mshiriki wa dini ambayo mafundisho yake hayaungi mkono kutumia silaha.”

Zaidi ya hilo, mahakama hiyo ya wilaya ilithibitisha kwamba Bw. Shalaiko ana haki ya kupewa utumishi wa badala “kwa msingi wa Katiba ya Ukrainia.” Pia ilieleza kuwa Mkataba wa Ulaya Kuhusu Haki za Kibinadamu c na hukumu za Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu (ECHR) zinatetea uhuru wa kidini. Hakimu alifuta mashtaka hayo dhidi ya Bw. Shalaiko. Mwendesha-mashtaka alikata rufani.

Rufani: Je, Haki ya Uhuru wa Dhamiri Isizingztiwe Wakati wa Vita?

Mwendesha-mashtaka huyo alisisitiza kwamba takwa la kikatiba la kulinda nchi ni la maana zaidi kuliko haki ya uhuru wa kidini na ya kufanya utumishi wa badala. Alisababu kwamba maamuzi ya ECHR hayapaswi kuzingatiwa wakati nchi ikiwa vitani.

Februari 26, 2015, Mahakama ya Rufani ya eneo la Dnipropetrovsk iliamua kwamba “kukataa utumishi wa jeshi wakati wa vita kwa sababu ya dhamiri si kukataa utumishi wa jeshi bila sababu za msingi.” Katika uamuzi wake, mahakama ilizingatia imani ya kidini ya Bw. Shalaiko na kurejelea maamuzi ya ECHR na kueleza kwamba “imani hizo za kidini zinatetewa katika Kipengele cha 9 cha Mkataba [wa Ulaya]” d kinachohusu uhuru wa kufikiri, dhamiri, na dini.

Mahakama hiyo ya rufani pia ilieleza kwamba Kipengele cha 9 cha Mkataba wa Ulaya Kuhusu Haki za Kibinadamu hakiruhusu “‘Usalama wa taifa’ . . . kuwa sababu ya kukiuka haki zinazopatikana humo.” Mahakimu walisababu kwamba “haki ya kukataa utumishi wa jeshi kwa sababu ya dhamiri haipaswi kudhibitiwa kwa sababu ya usalama wa taifa.” Walifikia mkataa kuwa sheria ya Ukrainia ya haki ya utumishi wa badala izingatiwe hata wakati nchi iko vitani. Ikiunga mkono uamuzi wa awali wa mahakama, mahakama hiyo ya rufani ilifuta mashtaka dhidi ya Vitaliy Shalaiko.

Kutumia Haki za Kibinadamu Si Uvunjaji wa Sheria

Maamuzi hayo ya mahakama yanatambua na kutetea haki ya kukataa utumishi wa jeshi kwa sababu ya dhamiri na ya kufanya utumishi badala wa kiraia—hata wakati wa dharura ya kitaifa. Maamuzi ya kesi ya Bw. Shalaiko yanaambatana na sheria za kimataifa zinazotambua haki ya msingi ya kukataa utumishi wa jeshi kwa sababu ya dhamiri. e

Hata hivyo, mwendesha-mashtaka amepeleka kesi hiyo kwenye Mahakama Kuu ya Ukrainia inayosikiliza kesi za kipekee (High Specialized Court of Ukraine for Civil and Criminal Cases) akiwa na hoja zilezile zilizojadiliwa na kupingwa na mahakama ya rufaa. Aprili 30, 2015, mwanasheria wa Bw. Shalaiko alipinga rufaa ya pili ya mwendesha-mashtaka.

Vitaliy Shalaiko ni miongoni mwa maelfu ya Mashihidi nchini Ukrainia walioitwa kufanya utumishi wa jeshi. Kwa heshima wanafika katika ofisi za jeshi na kuomba kufanya utumishi wa badala ambao haupingani na imani yao ya kidini. Mara nyingi maombi hayo hukubaliwa, na ni Mashahidi wachache waliofunguliwa mashtaka. Sasa mahakama kuu ya Ukrainia ndiyo itakayoamua ikiwa Ukrainia itaheshimu ombi la Mashahidi la kukataa utumishi wa jeshi kwa sababu ya dhamiri.

b Soma makala “Kwa Nini Hamwendi Vitani?

c Ukrainia ilikubali rasmi Mkataba wa Ulaya Kuhusu Haki za Kibinadamu mwaka wa 1997.

d Uamuzi wa mahakama ya rufaa ulirejelea kihususa hukumu za ECHR katika kesi ya Jehovah’s Witnesses of Moscow and Others v. Russia na Bayatan v. Armenia.

e Ona Bayatyan v. Armenia [GC], na. 23459/03, §§ 98-111, ECHR 2011; Jeong et al. v. Republic of Korea, UN Doc CCPR/C/101D/1642-1741/2007 (24 Machi 2011) §§ 7.2-7.4.