Hamia kwenye habari

AGOSTI 28, 2015
UKRAINIA

Mahakama Kuu ya Ukrainia Yatetea Haki ya Kutojiunga na Jeshi kwa Sababu ya Dhamiri Watu Wanapoandikishwa Kwenda Vitani

Mahakama Kuu ya Ukrainia Yatetea Haki ya Kutojiunga na Jeshi kwa Sababu ya Dhamiri Watu Wanapoandikishwa Kwenda Vitani

Mahakama kuu ya Ukrainia imesema kwamba watu wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri wana haki ya kufanya utumishi wa badala hata wakati wa vurugu za kisiasa na vita. Uamuzi huu utaathiri sana haki za binadamu, nchini Ukrainia na kwingineko.

Vitaliy Shalaiko, ambaye ni Shahidi wa Yehova, alisingiziwa kuwa amekataa kujiunga na jeshi wakati wa vita kwa sababu aliomba afanye utumishi wa badala alipoitwa ajiandikishe. Mahakama ya wilaya na mahakama ya rufaa zilimwondolea mashtaka, lakini mwendesha mashtaka alikata rufaa katika Mahakama Kuu ya Kesi za Jinai na za Madai. Juni 23, 2015, mahakama hiyo ilikataa rufaa ya mwendesha mashtaka, na hivyo kukamilisha uamuzi wa mahakama za chini.

Mahakama kuu imeunga mkono kwa kusema kwamba “mahakama ya wilaya ilifanya sawa kurejelea Mkataba wa Ulaya wa Haki za Binadamu na maamuzi ya Mahakama ya Ulaya ya Haki za Binadamu.” Pia ilikubaliana na mahakama ya wilaya kwamba uamuzi wa kesi ya Bayatyan dhidi ya Armenia ulifaa kutumiwa. Kesi hiyo iliamuliwa na Baraza Kuu la Mahakama ya Ulaya ya Haki za Binadamu mnamo Julai 7, 2011. Katika uamuzi huo wa kihistoria, mahakama hiyo iliamua kwamba kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri ikitegemea imani za dini kunatetewa na Kifungu cha 9 cha Mkataba wa Ulaya wa Haki za Binadamu. Katika kesi ya Vitaliy Shalaiko, mahakama kuu ya Ukrainia ilisema wazi kwamba haki za wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri zinalindwa hata wakati nchi inapokusanya watu wakapigane vitani na si tu katika utaratibu wa kawaida wa kuwaandikisha watu jeshini. Uamuzi wa mahakama hiyo kuu ndiyo wa mwisho, na hakuna rufaa yoyote itakayokubaliwa ili kupinga uamuzi huo.

Uamuzi huo wa mwisho umemwondolea wasiwasi Bw. Shalaiko. Anasema hivi: “Ninaelewa kwamba nchi yangu inataka kulinda raia zake kwa kuwakusanya watu wakapigane vitani. Ingawa dhamiri yangu hainiruhusu kutumikia jeshini, niko tayari kufanya utumishi wa badala wa raia. Ninashukuru sana kwamba mahakama zimetambua kwamba kukataa kwangu kujiunga na jeshi kunategemea kabisa mafundisho ya dini yangu.”

Uamuzi Unaowanufaisha Wengi

Maelfu ya Mashahidi wa Yehova nchini Ukrainia wamekabili suala la kutojihusisha na siasa wakati wa kuandikisha watu kwenda vitani. Wale wanaokabili mashtaka ya jinai kwa sababu ya kuepuka utumishi wa kijeshi, sasa wanaweza kutegemea uamuzi uliotolewa katika kesi ya Vitaliy Shalaiko.

Bw. Vadim Karpov, wakili wa Bw. Shalaiko alisema: “Kwa maneno rahisi, mahakama kuu inaeleza kwamba Bw. Shalaiko akiwa Shahidi wa Yehova hangeweza kuhukumiwa kwa sababu ya kukataa kujiunga na jeshi. Hata katika nchi kama Ukrainia, ambayo imegawanyika kwa sababu ya vita na machafuko, ni muhimu kwamba viwango vya sheria za kimataifa za uhuru wa ibada na uhuru wa dhamiri vimetumiwa.”

Ukrainia Yaweka Mfano Katika Kuheshimu Haki za Binadamu

Mahakama nchini Ukrainia zimetambua kwamba kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri ni haki ya msingi ya binadamu ambayo humlinda mtu hata wakati ambapo watu wanaandikishwa kwa ajili ya kwenda vitani. Mtu hafanyi hivyo kwa ubinafsi ili kuepuka wajibu na wala jambo hilo halihatarishi masilahi na usalama wa taifa. Kwa kuunga mkono uamuzi wa mahakama za chini, mahakama kuu imetetea haki za binadamu za raia wote wa Ukrainia. Ukrainia imeweka mfano kwa nchi nyingine ambazo zinawahukumu wale wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri zao.