Hamia kwenye habari

JULAI 10, 2015
UKRAINIA

Washambuliwa kwa Sababu ya Imani ya Dini Huko Mashariki mwa Ukrainia

Washambuliwa kwa Sababu ya Imani ya Dini Huko Mashariki mwa Ukrainia

Tangu Agosti 2014, vikundi vya watu wenye silaha huko Mashariki mwa Ukrainia vimewateka nyara na kuwatendea isivyo haki Mashahidi wa Yehova 26 kwa sababu ya chuki ya dini. Mashahidi wengi wanaishi eneo hilo, na wanajulikana sana kwa sababu ya kuhubiri hadharani na msimamo wao wa kutounga mkono upande wowote wa siasa. Kutokuwapo kwa sheria na utaratibu katika eneo hilo kumewanufaisha baadhi ya washiriki wa vikundi hivyo vya watu wenye silaha na kuwafanya wawashambulie kikatili Mashahidi. a

Matukio ya Jeuri

  • Mei 21, 2015, maofisa wa polisi katika mji wa Stakhanov waliwatia mbaroni wanaume wawili Mashahidi wenye umri wa miaka zaidi ya 60, kwa sababu ya kufanya shughuli za dini. Walishtakiwa kwa “kuvuruga amani” na wakahukumiwa kifungo cha siku 15. Wakiwa chini ya ulinzi wa polisi, Mashahidi hao wawili walishutumiwa kuwa ni wapelelezi na walihojiwa mara nyingi kuhusu tengenezo la Mashahidi wa Yehova. Washiriki wa kutaniko walimwomba mwendesha mashtaka wa eneo hilo awaachilie wanaume hao, lakini alikataa. Mwanzoni washiriki wa familia na Mashahidi wenzao walikatazwa kuwatembelea wanaume hao lakini hatimaye waliruhusiwa kuwapelekea chakula, mavazi na dawa mara tatu kwa juma. Shahidi mmoja aliachiliwa Juni 2, 2015, na mwenzake aliachiliwa siku iliyofuata—nao waliamriwa wahame eneo hilo.

  • Mei 17, 2015, wanaume wenye silaha katika eneo la Novoazovsk waliwakamata Mashahidi wanne, waliwafunga macho kwa vitambaa, na kuwapeleka katika makao makuu ya jeshi ya eneo hilo huku waliwaelekezea bunduki. Kwa saa mbili waliwapiga kikatili Mashahidi hao na kuwatishia kuwaua. Walimlazimisha Shahidi ambaye alikuwa mdogo kuliko wote ajiunge na jeshi lao na wale wengine wakiri kwamba Othodoksi ndiyo dini ya kweli. Mashahidi hao waliachiliwa baada ya kufungwa usiku mzima kwenye gereza la muda lililo na nafasi ndogo.

  • Baadhi ya majeraha waliyopata Mashahidi wawili waliotekwa nyara na kupigwa katika eneo la Novoazovsk

  • Januari 22, 2015, wanaume watatu wenye silaha walimkamata Shahidi mmoja aliyekuwa kwenye eneo lake la kazi huko Donetsk. Familia yake haikujua alikopelekwa wala sababu ya kukamatwa. Akiwa kizuizini, aliwaeleza mara kwa mara msimamo wake wa kutounga mkono siasa na baada ya siku tisa aliachiliwa.

  • Agosti 9, 2014, mwanamgambo aliyekuwa na silaha aliwateka nyara Mashahidi wawili huko Stakhanov, katika mkoa wa Luhansk. Mashahidi hao walioshikiliwa kwa siku sita, walipigwa sana, walitishiwa kukatwa viungo na kuuawa. Pia hawakupewa maji ya kutosha, chakula, nguo na matibabu. Watekaji nyara waliwalazimisha wakane imani yao, wakariri kanuni za imani ya Othodoksi, na kuabudu sanamu za kanisa hilo, mambo ambayo yalionyesha wazi kwamba kukamatwa kwao kulihusiana na dini. Licha ya kutendewa kwa ukatili, Mashahidi hao hawakulegeza msimamo wao.

Mashahidi wa Yehova wanaishi kulingana na mafundisho yao ya dini nao hawapigani, hawafanyi kampeni, wala kutoa mchango wa kifedha ili kuunga mkono upande wowote wa vita nchini Ukrainia. Vikundi vya watu wenye silaha vinawashambulia Mashahidi kwa sababu hawaungi mkono siasa na hawafuati mafundisho ya Othodoksi. Mashambulizi hayo yanafanywa ili kuwalazimisha Mashahidi wakane imani yao.

Kuvumilia licha ya Mateso

Mashahidi hawawezi kupata haki yao ya kisheria, kwa kuwa bado eneo hilo liko katika mzozo. Wamepeleka malalamiko yao kuhusu visa hivyo na vingine vinavyofanana kama hivyo kwenye mashirika ya kimataifa, kutia ndani Mwandishi Maalumu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia vitendo vya ukatili.

Licha ya kuvumilia hali ngumu wanazoweza kupata, Mashahidi wa Yehova huko mashariki mwa Ukrainia wanaendelea kutounga mkono siasa na kufanya ibada zao kwa busara. Wanatumaini kwamba wenye mamlaka watatekeleza haki ya msingi ya binadamu ya kuwa na uhuru wa ibada.

a Wanaume wenye silaha walimshambulia Yuriy, anayeonyeshwa kwenye picha ya mwanzoni, kwa sababu ni Shahidi wa Yehova. Katika kisa kimoja, walimsimamisha njiani alipokuwa akirudi kutoka katika shughuli za dini, na katika visa vingine viwili, walimshambulia alipokuwa nyumbani kwake. Walimwamuru akane imani yake na kuacha kushirikiana na Mashahidi wa Yehova.