Hamia kwenye habari

JANUARI 25, 2023
HABARI ZA ULIMWENGUNI POTE

JW.ORG Yatimiza Miaka 10—Sehemu ya 2

Kuhakikisha Undugu Wote Unapata Habari za Karibuni

JW.ORG Yatimiza Miaka 10—Sehemu ya 2

Sehemu ya kwanza ya mfululizo huu ilizungumzia jukumu la jw.org katika kusambaza video na machapisho kupitia mtandao. Sehemu ya pili itazungumzia jinsi jw.org imesaidia kuhakikisha undugu wa ulimwenguni pote unapata habari za karibuni kuhusu matukio yanayowaathiri Mashahidi wa Yehova.

Makala za Habari Zinazotolewa kwa Wakati: Kwa kawaida sehemu ya Habari za JW kwenye jw.org huonyesha makala za karibuni zilizo na habari zinazotegemeka kuwahusu ndugu zetu. Hilo linatia ndani habari za karibuni kuhusu misiba ya asili na jitihada za kutoa msaada, upinzani wa serikali, vifungo visivyo vya haki vya ndugu na dada zetu katika nchi mbalimbali, na matukio mengine muhimu. Kwa mfano, Machi 21, 2017, makala moja ilijulisha undugu wote kuhusu marufuku iliyokuwa karibu kutolewa dhidi ya ibada ya Mashahidi wa Yehova nchini Urusi na ikatia ndani mwaliko wa kuwaandikia barua maofisa wa serikali nchini Urusi.

Habari za Hivi Punde: Sehemu ya Habari za Hivi Punde ilitokea kwa mara ya kwanza kwenye jw.org mnamo Julai 2017. Taarifa hizo fupi hujulisha undugu wetu kuhusu matukio ya hivi punde bila kuandika makala nzima. Kwa mfano, taarifa huandikwa ndugu na dada zetu waliokuwa wamefungwa kwa ajili ya imani yao wanapoachiliwa. Kwa mfano, taarifa moja ilitolewa Desemba 31, 2020, Feliks Makhammadiyev alipoachiliwa kutoka gerezani nchini Urusi na kuunganishwa na mke wake, Yevgeniya. Wakati wa janga la COVID-19, Habari za Hivi Punde zilitumiwa kutangaza kutolewa kwa vipindi vya kusanyiko la eneo mtandaoni na pia kuwasilisha maamuzi muhimu yaliyofanywa na Baraza Linaloongoza la Mashahidi wa Yehova, kama vile kuanza tena kufanya mikutano ya uso kwa uso na kurudia tena huduma ya umma. Taarifa nyingi zimetolewa saa chache tu baada ya tukio muhimu kutokea upande mmoja wa ulimwengu. Kwa mfano, Juni 2018, taarifa ya Habari za Hivi Punde ilitolewa muda mfupi tu baada ya Mahakama ya Kikatiba ya Korea Kusini kufanya uamuzi wa kihistoria wa kutangaza kwamba ni ukosefu wa haki kwa nchi hiyo kukosa kuwa na uandalizi wa utumishi badala wa kiraia.

Ripoti za Baraza Linaloongoza: Machi 18, 2020, ripoti ya kwanza ya Baraza Linaloongoza ilitolewa kwenye jw.org kuandaa kitia-moyo wakati wa janga la COVID-19. Wengi wanahisi kama dada mmoja aliyesema hivi kuhusu ripoti hizo: “Ninahisi ni kama nimetembelewa kirafiki ili kunijulia hali. Sioni jinsi ambavyo ningefaulu kukabiliana na hali wakati wa janga bila kuwa na ripoti hizo. Sikuzote zilikuja kwa wakati unaofaa.” Jumla ya ripoti 28 zimetolewa kufikia sasa.

Kadiri ulimwengu unavyozidi kugawanyika na matukio muhimu yanatokea upesi, imekuwa vigumu hata zaidi kupata vyanzo vya habari vinavyoaminika. Lakini tunashukuru kwamba ndugu zetu wanaweza kupata habari kwa wakati na zilizo sahihi kwenye jw.org. Hilo linatusaidia sisi sote ‘kuendelea kuwa watulivu na kuwa na tumaini.’​—Isaya 30:15.

  • Video zinazopakuliwa kila mwezi

  • Watu wanaotembelea tovuti yetu kila mwezi

  • Tangazo kuhusu kampeni ya ulimwenguni pote ya kuandika barua, Machi 2017

  • Kutolewa kwa ripoti ya kwanza ya Baraza Linaloongoza, Machi 2020

  • Tangazo kuhusu kuanza tena kwa mikutano ya uso kwa uso, Machi 2020

  • Tangazo kuhusu kurudia tena mahubiri ya umma, Juni 2022

  • Kutolewa kwa makusanyiko ya eneo mtandaoni, Juni hadi Agosti, 2022