Hamia kwenye habari

NOVEMBA 14, 2019
HABARI ZA ULIMWENGUNI POTE

Kampeni ya Pekee kwa Ajili ya Watu Wanaozungumza Kiarabu Nchini Austria na Ujerumani

Kampeni ya Pekee kwa Ajili ya Watu Wanaozungumza Kiarabu Nchini Austria na Ujerumani

Kuanzia Agosti 31 hadi Oktoba 26, 2019, ndugu na dada kutoka nchi 19 walishiriki kutoa elimu ya Biblia katika lugha ya Kiarabu nchini Austria na Ujerumani. Wakati wote wa kampeni hiyo ya pekee, washiriki wote 1,782 walitumia jumla ya saa 40,724 ili kutoa elimu hiyo, walionyesha video 4,483, na kutoa machapisho 24,769.

Katika miaka kadhaa iliyopita, zaidi ya wakimbizi milioni moja wamekimbilia Austria na Ujerumani, wengi wao kutoka nchi zinazotumia lugha ya Kiarabu. Wengi wao hawajawahi kusikia ujumbe wenye kufariji wa Biblia. Ndugu na dada waliosafiri kutoka Kanada, Marekani, na baadhi ya nchi za Ulaya waliwaunga mkono wahubiri 1,108 wa nchi ya Austria na Ujerumani wanaotumikia katika eneo la watu wanaozungumza lugha ya Kiarabu. Walihubiri katika maeneo 24, kutia ndani miji mikubwa kama vile Berlin, Cologne, Dresden, Frankfurt, Graz, Hamburg, na Vienna.

Ndugu mmoja wa eneo hilo aliandika hivi: “Kampeni hii ilikuwa na matokeo mazuri kwetu, ambayo tusingeweza kuwazia. Ndugu waliotutembelea walituchochea, na tunashukuru sana kwa msaada wao. Tunashukuru sana kwa pendeleo la kushiriki katika kampeni hii ya pekee.”

Baada ya kuhudhuria mkutano wa Mashahidi wa Yehova, kijana mmoja kutoka nchi inayotumia lugha ya Kiarabu alimfuata ndugu mmoja na kumuuliza hivi kwa shauku: “Unajua neno mahabba linamaanisha nini kwa Kijerumani?”

Ndugu huyo akamjibu, “Liebe (upendo)!”

Kijana huyo akasema, “Ndiyo, hilo ndilo jambo ambalo nimejionea kwa matendo leo! Mmenionyesha fadhili nyingi. Kila mtu alinisalimu kwa mkono. Nimejionea watu kutoka nchi mbalimbali wakitendeana kwa heshima. Ikiwa kila mtu angetenda kwa njia hii, ulimwengu wote ungekuwa tofauti sana.”

Mwanamume mwingine alisema hivi kuwahusu Mashahidi wa Yehova: “Mna ustadi wa kuwasiliana na watu, na mmefanyiza mojawapo ya jamii bora zaidi ulimwenguni.”

Wenzi fulani kutoka nchi inayozungumza lugha ya Kiarabu ambao wameishi Ujerumani kwa mwaka mmoja hivi, waliwaalika akina ndugu nyumbani kwao kwa ajili ya chakula chepesi. Akina ndugu walipowaeleza sababu iliyowafanya wafike nyumbani kwao, mke aliuliza hivi, “Je, ninyi ni Mashahidi wa Yehova?” Akina ndugu waliposema kwamba wao ni Mashahidi, mwanamke huyo alisema: “Siamini! Nimekuwa nikiwatafuta kwa miezi kadhaa. Hata nilienda kuwatafuta kwenye kituo kikuu cha treni. Na sasa mko hapa. Nyinyi ndio mmekuja nyumbani kwangu! Mungu ndiye aliyewatuma.”

Yehova amebariki sana bidii ya ndugu na dada walioshiriki katika kampeni hiyo ya pekee ya kuwapa “watu wa mataifa yote” ujumbe wenye tumaini wa Biblia.—Mathayo 28:19.