AGOSTI 19, 2024
HABARI ZA ULIMWENGUNI POTE
Kimbunga Debby Kimesababisha Mafuriko Makubwa Kwenye Pwani ya Mashariki ya Amerika ya Kaskazini
Mwanzoni mwa Agosti 2024, dhoruba kubwa ilitokea katika bahari ya Atlantiki. Dhoruba hiyo iliongezeka ukubwa upesi na kusababisha Kimbunga Debby. Kisha Agosti 5, 2024, kimbunga hicho kilipiga eneo la karibu na Steinhatchee, Florida, Marekani, kikiambatana na upepo mkali uliovuma kwa kasi ya kilomita 130 kwa saa. Kwa kuongezea, kimbunga hicho kilitokeza dhoruba nyingine 12 popote kilipopita. Umeme ulikatika katika maeneo mengi sana kutokana na upepo mkali na mvua kubwa. Kibunga hicho kilisababisha vifo vya watu wanane hivi nchini Marekani.
Baadaye, kimbunga hicho kilipungua nguvu na kuelekea upande wa kaskazini hadi Kanada. Ijumaa, Agosti 9, 2024, jimbo la Quebec, Kanada lilipata mvua kiasi cha sentimeta 22 kwa muda wa chini ya saa 24. Mvua hiyo kubwa ilisababisha mafuriko makubwa katika nyumba za watu, ikaharibu miundo-msingi ya baadhi ya maeneo ya jimbo hilo, na kuwalazimisha mamia ya watu kukimbilia maeneo salama. Ripoti nchini Kanada zinaonyesha kwamba mtu mmoja alikufa.
Athari Ambazo Ndugu na Dada Zetu Wamepata
Marekani
Hakuna ndugu au dada ambaye amekufa
Mhubiri 1 alilazwa hospitali
Wahubiri 23 walilazimika kuhama makao yao
Nyumba 7 zilipata uharibifu mkubwa
Nyumba 60 zilipata uharibifu mdogo
Jumba 1 la Ufalme lilipata uharibifu mdogo
Kanada
Hakuna ndugu au dada ambaye amekufa. Hata hivyo, tunasikitika kuripoti kwamba mwanafunzi mmoja wa Biblia alikufa kutokana na poromoko la ardhi
Mhubiri 1 alijeruhiwa
Wahubiri 23 walilazimika kuhama makao yao, lakini wengi tayari wamerudi nyumbani
Nyumba 2 zilipata uharibifu mkubwa
Nyumba 165 zilipata uharibifu mdogo
Hakuna Jumba la Ufalme ambalo lilipata uharibifu
Jitihada za Kutoa Msaada
Waangalizi wa mzunguko na wazee wa makutaniko nchini Marekani na Kanada wanaandaa msaada wa kiroho na wa kimwili kwa wote walio katika maeneo yaliyoathiriwa
Nchini Kanada, Halmashauri ya Kutoa Msaada imeanzishwa ili kutoa msaada unaohitajika
Tunaendelea kusali kwa ajili ya wale walioathiriwa na kimbunga hicho na tunafarijika kujua kwamba Yehova hajawahi kushindwa kuwa “wokovu wetu wakati wa taabu.”—Isaya 33:2.