Hamia kwenye habari

Ndugu na dada kutoka sehemu mbalimbali barani Ulaya walifurahi kupokea kitabu cha Mathayo katika Kikurdi cha Kikurmanji na Kikurdi cha Kikurmanji (cha Caucasus)

JULAI 11, 2023
HABARI ZA ULIMWENGUNI POTE

Kitabu cha Mathayo Chatolewa Katika Kikurdi cha Kikurmanji na Kikurdi cha Kikurmanji (cha Caucasus)

Kitabu cha Mathayo Chatolewa Katika Kikurdi cha Kikurmanji na Kikurdi cha Kikurmanji (cha Caucasus)

Julai 2, 2023, Biblia—Habari Njema Kulingana na Mathayo ilitolewa katika lugha mbili za Kikurdi. Programu ya kwanza ilifanyika nchini Ujerumani, ambako kitabu hicho cha Biblia kilitolewa katika Kikurdi cha Kikurmanji, nacho kitabu cha Mathayo cha Kikurdi cha Kikurmanji (cha Caucasus) kilitolewa nchini Georgia. Jumla ya watu 750 hivi walihudhuria matukio yote mawili.

Kikurdi cha Kikurmanji

Ndugu Dirk Ciupek, mshiriki wa Halmashauri ya Tawi ya Ulaya ya Kati alitangaza kutolewa kwa kitabu cha Mathayo katika Kikurdi cha Kikurmanji kwenye programu iliyofanywa katika ofisi ya tawi ya Ulaya ya Kati jijini, Selters, Ujerumani. Wale waliohudhuria walipata nakala zilizochapishwa. Nakala za kielektroni pia zilipatikana.

Kikurdi cha Kikurmanji (cha Caucasus)

Ndugu Levani Kopaliani, mshiriki wa Halmashauri ya Tawi ya Georgia alitangaza kutolewa kwa kitabu cha Mathayo katika Kikurdi cha Kikurmanji (cha Caucasus) katika programu iliyofanyika jijini Tbilisi, Georgia. Ndugu na dada walio Aparan, Armavir, na Yerevan, nchini Armenia walisikiliza programu hiyo kupitia video iliyounganishwa mtandaoni. Wale waliohudhuria walipata nakala zilizochapishwa. Nakala za kielektroni pia zilipatikana.

Kikurdi cha Kikurmanji na Kikurdi cha Kikurmanji (cha Caucasus) ni lugha zinazofanana lakini zinatofautiana katika sarufi na muundo wa sentensi. Kwa kuongezea, ingawa baadhi ya maneno yanafanana yanaweza kuwa na maana tofauti. Kwa hiyo, watafsiri wa lugha zote mbili walishirikiana kwa ukaribu walipokuwa wakifanya kazi ya kutafsiri kitabu cha Mathayo. Mtafsiri mmoja alisema hivi kuhusu faida za kupata kitabu hiki cha Biblia: “Wakurdi wengi wana kiu kwa ajili ya kweli, tafsiri hii mpya itawaburudisha kama kunywa maji safi.”

Tunaungana pamoja na ndugu na dada zetu wanaozungumza Kikurdi cha Kikurmanji na Kikurdi cha Kikurmanji (cha Caucasus) kumshukuru na kumsifu Yehova kwa kuwafungulia watu wengi zaidi njia ya kutosheleza uhitaji wao wa kiroho!—Mathayo 5:3.