JULAI 27, 2021
HABARI ZA ULIMWENGUNI POTE
Mafuriko Makubwa Yatokea Magharibi mwa Ulaya
Mvua kubwa ilinyesha kuanzia Julai 13 hadi 17, 2021, na kusababisha mito mingi nchini Ubelgiji, Ujerumani, Luxembourg, na Uholanzi kujaa na kutokeza mafuriko hatari. Uharibifu uliosababishwa bado unakadiriwa. Hayo ndiyo mafuriko mabaya zaidi kutokea katika muda wa miaka 100 iliyopita.
Athari ambazo ndugu na dada zetu wamepata
Hakuna aliyejeruhiwa vibaya au kufa
Wahubiri 304 hivi walilazimika kuhama kutoka nyumbani kwao
Nyumba 100 hivi ziliharibiwa vibaya
Nyumba 242 hivi zilipata uharibifu mdogo
Majumba 11 ya Ufalme yaliharibiwa
Jitihada za Kutoa Msaada
Halmashauri 4 za Kutoa Msaada (DRC) ziliundwa; 1 nchini Ubelgiji, 2 nchini Ujerumani na Luxembourg, na 1 nchini Uholanzi
Kwa sasa, Halmashauri hizo zinapanga kazi ya kufanya usafi na marekebisho, kazi inayotia ndani kuondoa maji na matope ndani ya nyumba, na pia kufanya marekebisho ya dharura
Halmashauri hizo pamoja na wazee wa maeneo hayo wamepanga kuwe na makao ya muda na maji ya kunywa kwa ajili ya wale waliolazimika kuhama nyumbani kwao
Waangalizi wa mzunguko katika maeneo hayo wanawapa msaada wa kiroho na wa kihisia ndugu na dada walioathiriwa
Mikutano ya kutaniko inayofanywa kupitia mtandao bado inaendelea. Washiriki wa Halmashauri ya Tawi wanawatia moyo na kuwafariji wahubiri walioathiriwa
Jitihada zote za kutoa misaada zinafanywa kwa kuzingatia miongozo ya kujilinda na COVID-19
Wazee katika kutaniko moja nchini Uholanzi walimsaidia dada mmoja mwenye umri mkubwa kuhama. Baada ya hapo, ndugu hao walimpigia simu mwana wake ambaye si Shahidi wa Yehova kumjulisha kwamba mama yake alikuwa salama. Baadaye mwana huyo alimwambia mama yake: “Dini yako ni nzuri sana. Wanakutunza vizuri kweli!”
Kikosi kimoja cha zima-moto kilikuwa kikiwatazama ndugu zetu walipokuwa wakifanya kazi ya kutoa msaada. Kikosi hicho cha zima-moto kiliwapongeza ndugu hao kwa sababu walitumia vifaa vinavyofaa kujilinda na kwa sababu ya utaratibu wao. Vivyo hivyo, kikosi kingine cha zima-moto nchini Ujerumani kilivutiwa na utayari wa ndugu zetu kutii miongozo waliyowapa. Mmoja wao alisema hivi: “Laiti kungekuwa na kikosi kama hiki katika kila eneo.”
Ndugu na dada walioathiriwa wanalishukuru sana tengenezo kwa msaada waliopewa. Wanalishukuru pia Baraza Linaloongoza kwa kuwatia moyo watu wa Yehova wajitayarishe kwa ajili ya misiba ya asili. Zaidi ya yote, wanamshukuru Yehova ambaye huwafanya watu wake ‘waishi kwa usalama bila kuhangaishwa na woga wa msiba.’—Methali 1:33.