Hamia kwenye habari

Ndugu Viktor Stashevskiy

MACHI 30, 2021
HABARI ZA ULIMWENGUNI POTE

Mahakama ya Crimea Yamhukumu Ndugu Viktor Stashevskiy Miaka Sita na Nusu Gerezani

Mahakama ya Crimea Yamhukumu Ndugu Viktor Stashevskiy Miaka Sita na Nusu Gerezani

Hukumu

Machi 29, 2021, Mahakama ya Wilaya ya Gagarinskiy katika Jiji la Sevastopol, Crimea, ilimhukumu Ndugu Viktor Stashevskiy miaka sita na nusu gerezani. Viktor alipelekwa kizuizini mara moja kisha akahamishiwa mahabusu. Atakata rufaa uamuzi huo.

Maelezo Mafupi Kumhusu

Viktor Stashevskiy

  • Alizaliwa: 1966 (Kansk, Eneo la Krasnoyarsk, Urusi)

  • Maisha Yake: Alihamia Sevastopol, Crimea, mnamo 1983. Alistaafu kutoka kwenye jeshi la wanamaji mnamo 1993. Katika mwaka wa 2002 alifunga ndoa na Larisa. Wana binti wawili. Sikuzote amevutiwa na utata na mpangilio uliopo katika ulimwengu na alitaka kumfahamu Muumba. Kujifunza Biblia kumempa kusudi maishani. Alibatizwa na kuwa Shahidi wa Yehova mnamo 2004

Historia ya Kesi

Juni 4, 2019, maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa (FSB) walivamia nyumba kumi za Mashahidi wa Yehova jijini Sevastopol. Upekuzi katika baadhi ya nyumba uliendelea kwa saa nne hivi. Wakati huo, maofisa wa FSB hawakuwaruhusu akina ndugu na familia zao wanywe maji wala kutumia choo. Pia, maofisa hao walijaribu kuwaogopesha, wakiwatisha kwamba wataharibu mali zao na kuwapandikizia dawa za kulevya ili washtakiwe kwa uhalifu.

Ndugu Viktor Stashevskiy alikamatwa na kuwekwa jela usiku wote. Alishtakiwa kuwa “kiongozi wa shirika lenye msimamo mkali.” Ukweli ni kwamba ameshtakiwa kwa imani yake ya kidini, jambo ambalo linakiuka waziwazi haki yake ya kikatiba.

Viktor anasema kwamba kuwa na ratiba nzuri ya kusoma Biblia na kutafakari kumemsaidia kuwa jasiri na kuvumilia kwa shangwe. Anaimarishwa hasa na maneno ya Mfalme Daudi yaliyo kwenye Zaburi 62:5-8. Licha ya majaribu yote ambayo amekabili, Viktor anasema hivi: “Uhusiano wangu na Yehova umeimarika kwa sababu sikuzote amekuwa kando yangu na nimemkaribia kuliko mtu mwingine yeyote. Sijawahi kuwa na shaka lolote kwamba Yehova anaona hali yangu ngumu na tamaa yangu ya kuendelea kuwa mwaminifu kwake, na kwamba kwa wakati unaofaa, atanitetea kwa ajili ya jina lake kuu.”

Tunajua kwamba Yehova atamtegemeza na kumbariki Viktor, familia yake, na ndugu na dada zetu wote wanaovumilia mateso. Yehova ataendelea kuwa kimbilio na ngome yao.—Zaburi 91:2.