Hamia kwenye habari

Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu iliyoko Strasbourg, Ufaransa

AGOSTI 9, 2021
HABARI ZA ULIMWENGUNI POTE

Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu Yatoa Uamuzi Kumuunga Mkono Ndugu Rostom Aslanian

Ushindi wa Uhuru wa Ibada wa Transnistria

Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu Yatoa Uamuzi Kumuunga Mkono Ndugu Rostom Aslanian

Julai 13, 2021, Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu (ECHR) ilitoa uamuzi wa kumuunga mkono Ndugu Rostom Aslanian katika kesi iliyohusisha nchi ya Moldova na Urusi. Ndugu Aslanian alipinga uamuzi wa kumfunga gerezani uliotolewa na wenye mamlaka katika eneo la Transnistria (Jamhuri ya Pridnestrovskaia Moldavskaia) kwa sababu alikataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Ushindi huo unaweka msingi kwa ajili ya kesi nyingine ili kutetea haki ya uhuru wa ibada huko Transnistria.

Ingawa Transnistria inatambuliwa kimataifa kuwa sehemu ya Moldova, nchi ya Urusi inahusika pia katika mkataba wa kusimamia mipango ya ulinzi ya eneo hilo. Nchi zote mbili ni washirika wa Mkataba wa Ulaya wa Haki za Kibinadamu na wanapaswa kuheshimu uhuru wa dhamiri.

Mwaka wa 2010, Ndugu Aslanian aliandikishwa jeshini lakini akaomba apewe utumishi wa badala kwa msingi wa imani yake inayotegemea Biblia. Machi 29, 2011, ombi lake lilikataliwa naye akahukumiwa kifungo cha mwaka mmoja gerezani. Ndugu Aslanian alitumikia kifungo chake, lakini kesi yake iliwasilishwa mbele ya Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu.

ECHR ilipokuwa ikitoa hukumu, ilitaja maamuzi ya kesi za awali ili kuonyesha kwamba hakukuwa na msingi wa kisheria wa kumhukumu Ndugu Aslanian kwa kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Mahakama hiyo ilisema kwamba Urusi ilikuwa ikidhibiti mambo ya kijeshi, kiuchumi, na kisiasa ya Transnistria. Hivyo, Urusi ndiyo ililaumiwa kwa sababu ya mambo yaliyotendeka, si Moldova. ECHR ilisema kwamba wenye mamlaka walikiuka uhuru wa kidini wa Ndugu Aslanian kwa kumhukumu kifungo cha mwaka mmoja gerezani kwa msingi wa “kukwepa kuandikishwa” na kwamba serikali inapaswa kumlipa fidia kwa ajili ya mwaka aliotumia gerezani.

Tunashangilia kwa sababu ya ulinzi wa kisheria ambao ndugu zetu wa Transnistria wanapata kutokana na uamuzi huo. Kwa mara nyingine tunahakikishiwa upendo mshikamanifu wa Yehova na kwamba atawatunza watu wake kwa upendo wanapokabili majaribu.—Zaburi 18:25.