Hamia kwenye habari

Picha ya jinsi Ramapo itakavyoonekana baada ya kukamilika

APRILI 27, 2022
HABARI ZA ULIMWENGUNI POTE

Mradi wa Makao Makuu wa Ramapo

Maofisa Waidhinisha Marekebisho ya Barabara ya Kuingia Ramapo; Idhini ya Mwisho ya Ramani Bado Inasubiriwa

Maofisa Waidhinisha Marekebisho ya Barabara ya Kuingia Ramapo; Idhini ya Mwisho ya Ramani Bado Inasubiriwa

Machi 8, 2022, Halmashauri ya Mradi wa Ujenzi wa Ramapo (CPC) ilipokea idhini kutoka kwa Kamati ya Mipango ya Mji wa Tuxedo. Idhini hiyo inawawezesha kuanza kazi ya kupanua na kurekebisha barabara ya kuingia Ramapo. Zaidi ya hilo, akina ndugu wanaendelea kufuatilia kibali cha mwisho cha kuidhinisha ujenzi huo kutoka kwa Kamati ya Mipango ya Mji wa Ramapo. a

Ndugu Robert McRedmond, ambaye ni mratibu wa halmashauri hiyo, alisema: “Punde tu baada ya kuanza mradi huu tuligundua kwamba tulihitaji kurekebisha barabara ya kuingia kwenye eneo la mradi. Kibali tulichokipata hivi karibuni kitaturuhusu kuwapa wakandarasi kazi ya kurekebisha barabara hivi kwamba magari yatapishana kwa usalama. Kazi hiyo inafanywa na wakandarasi na kufikia majira ya joto itakuwa imemalizika. Pia, wajitoleaji wa ujenzi wanamalizia kurekebisha daraja la mawe lililo kwenye barabara hiyo.”

Daraja la mawe linaloendelea kurekebishwa lililo karibu na eneo la mwingilio wa mradi

Ndugu Gary Stradowski, anayefanya kazi kwenye halmashauri hiyo, anasema hivi: “Tulifurahi sana tulipopata kibali hiki. Tunakaribia kufikia lengo letu la kupata kibali cha ramani ya mradi wote. Mara tu baada ya kupewa idhini wakandarasi wataanza kutengeneza uwanja na kuuandaa kwa ajili ya ujenzi, ikiwezekana kufikia mwishoni mwa mwaka wa 2022. Hilo likitukia, basi wajitoleaji wataanza kusaidia kwenye mradi huu kuanzia katikati ya mwaka wa 2023.”

Tunafurahi kupata habari hizi za karibuni na tunasali roho ya Yehova iendelee kuongoza mradi huu.​—Zekaria 4:6.

a Eneo la mradi la Ramapo limeanzia jimbo la Orange hadi jimbo la Rockland, New York, Marekani. Hivyo basi, Halmashauri ya Mradi wa Ujenzi inahitaji kupata vibali kutoka kwa Kamati ya Mipango ya Mji wa Tuxedo na Kamati ya Mipango ya Mji wa Ramapo.