Hamia kwenye habari

NOVEMBA 7, 2023
HABARI ZA ULIMWENGUNI POTE

Miaka Mia Moja Imepita Tangu Gazeti la Mnara wa Mlinzi Lianze Kuchapishwa Katika Kireno

Miaka Mia Moja Imepita Tangu Gazeti la Mnara wa Mlinzi Lianze Kuchapishwa Katika Kireno

Mwaka wa 1923, Ndugu George Young alienda nchini Brazili ili kuanzisha ofisi ya tawi na kupanga kazi ya kuhubiri. Wakati huo ni toleo la Kiingereza la The Watch Tower and Herald of Christ’s Presence tu (ambalo kwa sasa linajulikana kama Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova) lililopatikana nchini Brazili. Ndugu Young alifanya mipango haraka ili gazeti la Mnara wa Mlinzi litafsiriwe katika Kireno na kuchapishwa katika nchi hiyo. Matokeo ni kwamba toleo la kwanza la gazeti la Mnara wa Mlinzi lilipatikana Oktoba 1923 katika Kireno. Miaka mitatu baadaye, ofisi ya tawi ilipata mashine ya uchapishaji iliyotoka kwenye Makao Makuu ya Ulimwenguni Pote ya Mashahidi wa Yehova yaliyokuwa Brooklyn, New York, Marekani, na akina ndugu katika ofisi ya tawi ya Brazili wakaanza kuchapisha machapisho wao wenyewe.

Kushoto: Mashine ya kwanza ya uchapishaji iliyotumiwa katika ofisi ya tawi ya Brazili. Kulia: Toleo la kwanza la Mnara wa Mlinzi lililochapishwa katika Kireno kwenye ofisi ya tawi ya Brazili

Toleo la kwanza la Mnara wa Mlinzi lililochapishwa katika Kireno nchini Ureno, mwaka wa 1925

Miaka miwili baada ya toleo la kwanza la Kireno la Mnara wa Mlinzi kuchapishwa nchini Brazili, akina ndugu nchini Ureno walianza kutafsiri Mnara wa Mlinzi katika Kireno kinachozungumzwa barani Ulaya mwaka wa 1925. Hata hivyo, katika mwaka wa 1933, Mashahidi walianza kukabili upinzani mkali wakati ambapo kulikuwa na utawala wa kidikteta. Muda mfupi baada ya hapo kazi ya kutafsiri katika Kireno ilipigwa marufuku. Kuanzia wakati huo na kuendelea ndugu na dada nchini Ureno walikuwa wakitumia gazeti la Mnara wa Mlinzi la Kireno lililokuwa likichapishwa nchini Brazili. Dada anayeitwa Isabel aliyekuwa akiishi nchini Ureno wakati huo, anasema hivi: “Badala ya kukazia tofauti iliyopo kati ya lugha hiyo na lugha yetu au maana ya maneno mbalimbali, niliamua kukazia fikira ujumbe ili uingie moyoni. Ninawashukuru sana ndugu na dada nchini Brazili kwa kutusaidia kupata machapisho katika lugha ya Kireno ilipokuwa vigumu kwetu kupata machapisho katika lugha yetu wenyewe.”

Mwaka 1961, toleo la Kiingereza la Tafsiri ya Ulimwengu Mpya lilipotolewa, idhini ilitolewa ili kutafsiri Biblia hiyo katika lugha nyingine sita kutia ndani Kireno. Ingawa haikuwa rahisi, kikundi kilichotafsiri Biblia hiyo katika Kireno nchini Brazili kilikuwa na lengo la kutumia maneno ambayo watu wote wanaozungumza Kireno kutoka katika mataifa mbalimbali wangeweza kuelewa kwa urahisi. Kwa miaka mingi, kanuni hizo ziliendelea kutumiwa katika kutafsiri Mnara wa Mlinzi. Hata hivyo, katika mwaka wa 2017, idhini ilitolewa ili kutafsiri Mnara wa Mlinzi katika Kireno (cha Brazili) na pia katika Kireno (cha Ureno).

Kuanzia juu kushoto: Ndugu na dada wakihubiri habari njema kwa kutumia chapisho la Mnara wa Mlinzi iliyo katika Kireno nchini Angola, Brazili, Ureno, na Msumbiji

Kufikia sasa kuna wahubiri milioni 1.2 wanaozungumza Kireno ulimwenguni pote na inakadiriwa kwamba watu milioni 260 hivi wanazungumza lugha ya Kireno na wanaweza kunufaika kwa kutumia gazeti la Mnara wa Mlinzi katika lugha yao wenyewe. Tunasali kwamba watu hawa na wengine ulimwenguni pote waendelee kujifunza “kuhusu mambo makuu ya Mungu.”​—Matendo 2:11.