DESEMBA 21, 2023
HABARI ZA ULIMWENGUNI POTE
Ujenzi wa Kituo Kipya cha Utegemezo wa Kazi ya Mashahidi wa Yehova Waidhinishwa Huko Fishkill
Oktoba 27, 2023, ramani iliidhinishwa kwa ajili ya ujenzi wa majengo mapya ya Betheli katika mji wa Fishkill, New York, Marekani. Idhini hii iliyotolewa na Kamati ya Mipango ya Mji inaruhusu kazi ya ujenzi wa majengo mapya ya Kituo cha Fishkill cha Kuandaa Utegemezo wa Kazi ya Mashahidi wa Yehova ianze mara moja.
Majengo hayo ya Betheli ya Fishkill yako kilomita 64 upande wa kaskazini wa Makao Makuu ya Mashahidi wa Yehova ya Warwick, New York, Marekani. Ndugu na dada walioko Fishkill wanatumikia katika idara za kuandaa utegemezo wa kompyuta, teknolojia ya habari, na migawo mingine.
Ujenzi huo mpya utafanywa kwenye eneo lenye ekari 23 upande mwingine wa barabara kutoka kwenye majengo ya sasa ya Betheli. Kutakuwa na jengo la ofisi lenye orofa moja litakalokuwa na urefu wa mita 4,366 za mraba, jengo la idara ya udumishaji lenye urefu wa mita 1,393 za mraba, na jengo la michezo lenye urefu wa mita 1,393 za mraba. Pia, kutakuwa na sehemu ya nje kwa ajili ya michezo mingine. Kila kitu kimebuniwa kwa njia ambayo hakutakuwa na uharibifu wa mazingira.
Ingawa kazi nyingi ya ujenzi itafanywa na makampuni binafsi, mradi huo utasimamiwa na ndugu wachache wanaotumikia Betheli. Mradi huo unatarajiwa kukamilika kufikia Oktoba 2025.
Ndugu Jason Kahle, anayeishi Fishkill na kufanya kazi katika ofisi hiyo ya kuandaa utegemezo anasema hivi: “Kufikia sasa, Betheli ya Fishkill ni majengo ya makazi tu, hamna sehemu za kukutana pamoja. Hata hivyo, majengo hayo mapya yatafanya iwezekane kwa wengi wetu kukutana na kufanya kazi pamoja. Tunatazamia kwa hamu mradi huu utakapokamilika!”
Tunashangilia kupata tangazo kuhusu mradi huu mpya wa ujenzi ambao utawaunganisha zaidi wale wanaotumikia katika Betheli ya Fishkill. Tunasali pamoja nao kwamba Yehova abariki mradi huu wenye kusisimua.—Zaburi 127:1.