Hamia kwenye habari

SEPTEMBA 27, 2018
HABARI ZA ULIMWENGUNI POTE

Martin Boor: Aondolewa Mashtaka na Slovakia Miaka 90 Baada ya Kufungwa

Martin Boor: Aondolewa Mashtaka na Slovakia Miaka 90 Baada ya Kufungwa

Septemba 18, 2015, mahakama nchini Slovakia ilimwondolea mashtaka Martin Boor, ambaye alikuwa amehukumiwa kuwa mhalifu kwa sababu ya msimamo wake wa kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Uamuzi huo umetolewa miaka 90 baada ya hukumu ya Ndugu Boor, na hivyo kufanya hiyo kuwa kesi ya zamani zaidi ya mtu aliyekataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri kutanguliwa.

Msimamo wa Ujasiri Wamfanya Afungwe

Picha ya Martin Boor alipokamatwa.

Martin alikuwa mtu mwenye bidii wa International Bible Students, kama Mashahidi wa Yehova walivyojulikana wakati huo, mwaka wa 1920 alipokuwa na umri wa miaka 17. Oktoba 1924, aliandikishwa jeshini. Imani yake ilimchochea kukataa kushiriki utendaji wowote wa kijeshi au kula kiapo cha jeshi. Kwa sababu hiyo, maofisa walishuku utimamu wa akili yake na wakaagiza afanyiwe uchunguzi wa kiakili. Wachunguzi wa Ndugu Boor waligundua kwamba yeye ni timamu kiakili na pia kwamba “imani yake ya kidini haitegemei mambo ya kuwaziwa tu.”

Kwa kuwa Martin alikuwa timamu, Aprili 2, 1925, mahakama iliamua kwamba kukataa kwake kujiunga na jeshi kulikuwa uhalifu mkubwa. Kijana huyo aliyeoa alikabili kwa ujasiri hukumu iliyotolewa na mahakama: kifungo cha miaka miwili kilichohusisha hatua kali kama kifungo cha upweke na kunyimwa chakula. Hata hivyo, Martin hakumaliza kifungo chake chote. Agosti 13, 1926, aliachiliwa kwa sababu ya tabia yake nzuri akiwa gerezani.

Uamuzi wa ECHR Wawezesha Kuondolewa Mashtaka

Ndugu Boor alikufa Januari 7, 1985. Washiriki wa familia yake waliobaki waliomba aondolewe mashtaka kwa mara ya kwanza mwaka wa 2004 bila mafanikio. Miaka saba baadaye, waliomba kwamba Mahakama ya Mkoa wa Bratislava I ianzishe upya kesi hiyo baada ya Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu (ECHR), kutoa uamuzi katika kesi ya kihistoria ya Bayatyan dhidi ya Armenia, kwamba Mkataba wa Ulaya Kuhusu Haki za Kibinadamu unalinda wale wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Inasikitisha kwamba licha ya kuwa na msingi thabiti wa kisheria wa kutangua hukumu ya Martin, ombi la kuondolewa mashtaka halikuchukuliwa hatua yoyote na mahakama za chini. Mabadiliko yalitokea baada ya kesi ya mwingine aliyekataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri.

Uamuzi Muhimu Sana: Kesi ya Vajda

Kama Martin Boor, Imrich Vajda pia ni Shahidi wa Yehova aliyekataa utumishi wa kijeshi. Alihukumiwa kifungo katika mwaka wa 1959 na 1961 katika utawala wa Kikomunisti. Machi 13, 2014, Mahakama ya Kikatiba ilitoa uamuzi kwamba anapaswa kuondolewa mashtaka kwa msingi wa Sheria ya Czechoslovak Na. 119/1990 Coll. kuhusu kurekebisha maamuzi ya kihukumu (kuondoa mashtaka)—sheria ambayo kihususa imekusudiwa kushughulikia hukumu zilizotolewa na utawala wa Kikomunisti. Katika kesi ya Imrich Vajda, Mahakama ya Kikatiba ilieleza kwa mara ya kwanza jinsi Slovakia ilivyopaswa kutumia uamuzi uliotolewa na ECHR katika kesi ya Bayatyan kwa kukubali kwamba msamaha au kulipa ni hatua muhimu ya kisheria kwa wale waliohukumiwa kuwa wahalifu kwa kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri.

Uamuzi wa Vajda ulikuwa wa kwanza ulioruhusu ombi la Martin Boor lipelekwe kwenye Mahakama ya Mkoa wa Bratislava I ili aondolewe kabisa mashtaka. Mahakama ilikubali ombi lao Septemba 18, 2015. Hivyo, miaka 90 baada ya kuhukumiwa na miaka 30 baada ya kifo chake, Martin Boor ameondolewa mashtaka ya uhalifu kwa kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri.

Hivyo, uamuzi wa ECHR katika kesi ya Bayatyan na uamuzi wa Mahakama ya Kikatiba katika kesi ya Vajda umesaidia kurekebisha ukosefu huo wa haki wa muda mrefu. Kufikia sasa, Mashahidi wa Yehova 51—wengi wao walikuwa wamehukumiwa kuanzia mwaka wa 1948 hadi 1989—wameondolewa mashtaka kabisa na mahakama za Slovakia.