OKTOBA 9, 2014
HABARI ZA ULIMWENGUNI POTE
Mashahidi wa Yehova Wakabiliana na Janga la Ebola
NEW YORK—Ugonjwa mbaya sana wa Ebola unapoendelea kuangamiza watu katika Afrika Magharibi, Mashahidi wa Yehova wanaendelea kuwaelimisha washiriki wao kuhusu ugonjwa huo.
Mara tu ilipojulikana kwamba ugonjwa wa Ebola ulikuwa umeanza nchini Guinea na ulikuwa ukienea haraka nchini Liberia na Sierra Leone, ofisi za tawi za Mashahidi wa Yehova katika nchi hizo tatu zilituma barua ili kutahadharisha makutaniko yote yaliyo katika nchi hizo. Barua hizo, zilizotia ndani maagizo na mapendekezo ya mashirika ya serikali, zilieleza hatari ya virusi vya ugonjwa huo, jinsi unavyoenezwa, na hatua zinazoweza kuchukuliwa ili ugonjwa huo usiendelee kuenea. Collin Attick, msemaji wa Mashahidi wa Yehova nchini Sierra Leone anasema: “Kwa kuwa wengi katika eneo hili hawaelewi vizuri kuhusu magonjwa ya kuambukiza na pia kwa sababu ya kuenea kwa habari za uwongo kuhusu chanzo cha ugonjwa wa Ebola, watu wengi hawakujua la kufanya. Lakini washiriki wa makutaniko yetu waliposikia maagizo yaliyotolewa katika Majumba ya Ufalme, waliitikia vizuri na kutenda haraka.”
Mnamo Julai, wawakilishi wanaosafiri wa Mashahidi wa Yehova walifanya ziara za pekee za siku mbili katika kila kutaniko nchini Sierra Leone na Guinea. Katika ziara hizo, walitoa hotuba yenye kichwa “Utii Huokoa Uhai,” kusudi likiwa kuwaelewesha watu kuhusu jinsi ya kujilinda dhidi ya ugonjwa huo na vilevile kuwatia moyo wote waendelee kufuata miongozo ya karibuni zaidi waliyopewa. Ziara hizo zitaendelea hadi Novemba 2014. Isitoshe, kwenye mwingilio wa sehemu zao za ibada (zinazoitwa Majumba ya Ufalme) nchini Guinea, Liberia, na Sierra Leone, Mashahidi waliandaa vituo vya kunawia mikono vilivyo na maji yaliyochanganywa na kemikali za kuua viini. Mashahidi wengi katika nchi hizo wanaiga kielelezo hicho na kuandaa mahali pa kunawa mikono nje ya nyumba zao.
Kulingana na ripoti ya Oktoba 1, 2014 ya Shirika la Afya Ulimwenguni, kumekuwa na visa 7,178 vilivyoripotiwa vya ugonjwa huo na zaidi ya watu 3,300 wamekufa kutokana na ugonjwa wa Ebola ulioanza hivi karibuni katika Afrika Magharibi, na huenda idadi hiyo ikaongezeka. Kufikia Oktoba 2, kati ya Mashahidi wote 2,800 nchini Guinea na Sierra Leone, ni dada mmoja tu aliyekufa. Shahidi huyo aliyekuwa mwuguzi aliambukizwa ugonjwa huo na akafa Septemba 25, 2014. Kati ya Mashahidi 6,365 nchini Liberia, 10 wamekufa kutokana na ugonjwa huo; 6 kati yao walifanya kazi hospitalini. Ingawa hivi karibuni virusi vya ugonjwa huo vimeanza pia kuenea nchini Nigeria, hakuna Shahidi nchini humo ambaye ameambukizwa ugonjwa huo. Isitoshe, hakuna Shahidi mmishonari katika nchi hizo ambaye ameambukizwa; ugonjwa huo ulipoanza kuenea, baadhi ya wamishonari hao walikuwa wameenda likizo au walikuwa wakihudhuria makusanyiko barani Ulaya na Marekani. Wengine wao wamerudi hivi karibuni katika migawo yao ya umishonari na wanafuata maagizo na kutii tahadhari zote zinazotolewa na ofisi za tawi katika nchi wanamoishi. Wamishonari wengine bado hawajarudi kwa sababu ya vizuizi vya usafiri au kwa sababu nyingine.
Halmashauri za kuandaa msaada za Mashahidi waliojitolea zinawasaidia Mashahidi katika nchi za Afrika Magharibi zilizoathiriwa sana na Ebola kushughulikia mahitaji ya familia zao na ya waabudu wenzao. Thomas Nyain, Sr., msemaji wa Mashahidi wa Yehova nchini Liberia anasema: “Kufuata viwango vya Biblia vya usafi na vya kuwatenga wagonjwa kumesaidia kukabiliana na hali hii. Pia, tukiwa Mashahidi wa Yehova sisi huepuka desturi za mazishi zisizo za kimaandiko. Kufanya hivyo kumethibitika kuwa ulinzi kwa washiriki wetu wote, hasa katika kipindi hiki kigumu.”
Nchini Sierra Leone, kituo kimoja cha redio kilitangaza jinsi Mashahidi wa Yehova walivyowasaidia waamini wenzao na pia watu ambao si Mashahidi katika jamii ili kuepuka kuambukizwa virusi vya ugonjwa wa Ebola. Vilevile, wenye mamlaka waliomba halmashauri za kutoa msaada za Mashahidi zisaidie mashirika ya serikali katika eneo hilo.
Msemaji wa kimataifa wa Mashahidi katika makao makuu ya Mashahidi wa Yehova yaliyoko New York, J. R. Brown, alisema hivi: “Tunatiwa moyo kuona waamini wenzetu katika Afrika Magharibi wakijihadhari huku wakiendelea na utendaji wao wa kiroho na kazi ya elimu ya Biblia kwa kadiri wanavyoweza. Tunawafikiria na pia tunasali kwa ajili ya ndugu na dada zetu wa kiroho na watu wengine wanaokabiliana na athari za virusi vya ugonjwa huu wa Ebola.”
Wanahabari Wanaweza Kuwasialiana na:
J. R. Brown, Ofisi ya Habari za Umma, simu +1 718 560 5000
Guinea: Thierry Pourthié, tel. +224 631 40 96 50
Liberia: Thomas Nyain, Sr., tel. +231 886 513 414
Nigeria: Paul Andrew, tel. +234 7080 662 020
Sierra Leone: Collin Attick, tel. +232 77 850 790