SEPTEMBA 24, 2018
HABARI ZA ULIMWENGUNI POTE
Madhara ya Tufani Mangkhut
Kwa muda wa siku kadhaa, Tufani Mangkhut imesababisha uharibifu mkubwa katika eneo la magharibi ya Bahari ya Pasifiki na Bahari ya Kusini ya China. Ripoti zifuatazo zimetolewa na ofisi za tawi zinazowatunza ndugu na dada zetu walioathiriwa na janga hili.
Micronesia: Tufani Mangkhut ilipiga eneo la Rota, kisiwa kilicho sehemu ya Visiwa vya Kaskazini vya Mariana, Septemba 10, 2018. Ni dhoruba kali zaidi kupiga Rota tangu mwaka wa 2002. Tunafurahi kuripoti kwamba hakuna ndugu yeyote aliyeumia na ni jumba moja tu la Ufalme lililoathiriwa kisiwani humo. Ndugu mmoja alilazimika kuhama kwa muda mfupi ili nyumba yake irekebishwe. Tangu wakati huo mwangalizi ametembelea kisiwa hicho ili kuwatia moyo akina ndugu.
Ufilipino: Septemba 15, 2018, Tufani Mangkhut (wenyeji wanaiita “Ompong”) ilipiga eneo la Baggao, katika mkoa wa Cagayan, Ufilipino. Mangkhut ni dhoruba kali zaidi kupiga Ufilipino mwaka huu. Idadi ya vifo inayozidi kuongezeka imefikia 81.
Inasikitisha kwamba kwa sababu ya Tufani Mangkhut, dada mmoja kutoka Benguet alikufa na ndugu wanne walipata majeraha. Ripoti za awali zinaonyesha kwamba nyumba 938 za ndugu zetu zimeharibiwa kwa kiasi fulani na 15 zimeharibiwa kabisa. Majumba 28 ya Ufalme yameharibiwa, jumba moja lilikuwa karibu kuzamishwa kabisa na maporomoko ya ardhi. Halmashauri Nne za Kutoa Msaada (DRCs), katika maeneo ya Baguio, Cauayan, Laoag, na Tuguegarao, zinatunza mahitaji ya kimwili, kihisia, na kiroho ya ndugu na dada zetu. Katika siku zijazo, mshiriki wa Halmashauri ya Tawi atawatembelea akina ndugu kuwatia moyo.
Hong Kong: Tufani Mangkhut ilipiga eneo la Hong Kong Septemba 16, 2018. Ilisababisha madhara madogo kwenye ofisi ya tawi na kwenye jengo fulani linalotumiwa kama makazi ya Wanabetheli. Nyumba mbili za Mashahidi ziliharibiwa vibaya. Nyumba moja iliangukiwa na mti na nyingine paa iliezuliwa na upepo mkali. Nyumba nyingine chache ziliathiriwa na maji. DRC nchini Hong Kong inatunza mahitaji ya akina ndugu.
Tunawafikiria ndugu na dada zetu walioathiriwa na Tufani Mangkhut na kusali kwa ajili yao. Tunapata faraja kujua kwamba waabudu wenzetu wanawasaidia kwa upendo ndugu wenye uhitaji. Kwa kweli, familia yetu ya kiroho yenye umoja ni baraka kutoka kwa Yehova.—Methali 17:17.