Hamia kwenye habari

Ndugu Aleksandr Parkov akipokewa na mke wake, Galina, baada ya kuachiliwa kutoka gerezani

AGOSTI 13, 2024
URUSI

Aleksandr Parkov Ameachiliwa Kutoka Gerezani Nchini Urusi

Aleksandr Parkov Ameachiliwa Kutoka Gerezani Nchini Urusi

Agosti 9, 2024, Ndugu Aleksandr Parkov aliachiliwa kutoka gerezani nchini Urusi. Julai 29, 2021 alihukumiwa kifungo cha gerezani cha miaka sita na nusu. Kwa msingi wa muda ambao Aleksandr alitumia akiwa mahabusu kabla ya kufungwa, hukumu yake imekamilika.

Aleksandr na mke wake, Dada Galina Parkova, walitenganishwa kwa jumla ya zaidi ya miaka mitano. Katika kipindi hicho, Galina alihukumiwa kifungo cha nje cha miaka miwili na miezi mitatu katika kesi tofauti. Pia, alipoteza kazi yake kwa sababu ya kesi hiyo.

Alipokuwa gerezani, Aleksandr aliruhusiwa kuwasiliana na mke wake kwa kumpigia simu na kumwandikia barua. Galina anakumbuka jinsi alivyoendelea kumtia moyo kuvumilia hali ngumu: “Alinikumbusha mara nyingi kwamba maadamu Yehova yuko pamoja nasi, hatuna jambo la kuogopa.”

Tuna uhakika kwamba Yehova atawabariki Aleksandr na Galina wanapounganishwa tena na kuendelea kumwabudu pamoja. Sisi pia tutaendelea “kukesha kuhusiana na sala” kwa niaba ya wote ambao wamefungwa kwa ajili ya imani yao.​—1 Petro 4:7.