DESEMBA 21, 2022
URUSI
Baraza la Ulaya Lahimiza Urusi Kuondoa Marufuku Dhidi ya Mashahidi wa Yehova
Desemba 9, 2022, Katibu Mkuu wa Baraza la Ulaya (COE) alituma barua kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi na kuihimimza nchi hiyo kutekeleza maamuzi ambayo yalitolewa hivi karibuni na Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu (ECHR). Maamuzi hayo yanatia ndani uamuzi muhimu uliofanywa Juni 2022, ambao ulitangaza kwamba marufuku ya Urusi dhidi ya Mashahidi wa Yehova ni kinyume na sheria. a
Barua hiyo iliikumbusha nchi ya Urusi kwamba hata ingawa iliacha kuwa mwanachama wa Baraza la Ulaya Machi 2022, bado ina wajibu wa kutekeleza maamuzi yaliyotolewa na Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu, Septemba 16, 2022, au kabla ya hapo. Isitoshe, Halmashauri ya Mawaziri wa Baraza la Ulaya itaendelea kufuatilia kutekelezwa kwa maamuzi ya Mahakama hiyo.
Tangu uamuzi wa Juni 2022 ulipotolewa, Halmashauri hiyo imeihimiza sana Urusi kufutilia mbali uamuzi wa kupiga marufuku utendaji wa kidini wa Mashahidi wa Yehova ambao Mahakama Kuu ya Urusi ilifanya mwaka wa 2017. Halmashauri hiyo imeiagiza nchi ya Urusi “kufikiria upya sheria yake kuhusu msimamo mkali ambayo ndio msingi wa kutangaza mashirika ya Mashahidi wa Yehova kuwa yenye msimamo mkali . . . ; isimamishe uchunguzi na kesi zote za uhalifu dhidi ya Mashahidi wa Yehova na kuwaachilia Mashahidi ambao wamefungwa, ifutilie mbali mashtaka ya uhalifu na madhara ambayo yamesababisha, na pia irudishe mali zinazomilikiwa na Mashahidi ambazo serikali imetaifisha au ilipe fidia kwa ajili ya mali hizo.” b
Kufikia sasa, zaidi ya akina ndugu na dada 660 wamekabili matatizo ya kisheria kwa sababu ya marufuku hayo, licha ya kwamba wanafanya ibada yao kwa amani. Zaidi ya ndugu na dada 360 kati ya hao waliotajwa hapo juu, wamefungwa kipindi fulani kutia ndani ndugu na dada 114 ambao kwa sasa wako gerezani au mahabusu.
Zaidi ya ndugu na dada 450 wameongezwa kwenye orodha ya Urusi ya watu wenye msimamo mkali na magaidi, na hilo linafanya maisha yao na ya familia zao kuwa magumu. Orodha hiyo inapatikana kwa umma, hivyo ndugu na dada zetu wanadhaniwa kuwa wahalifu na inakuwa vigumu kwao kupata kazi. Pamoja na hilo, wanakabili matatizo mengine kutia ndani kuzuiwa kutumia akaunti zao za benki, ugumu wa kupata bima, kuuza mali, kuendesha uwekezaji, kupata urithi, au hata kununua tu kadi ya simu.
Tunafurahi kujua kwamba Baraza la Ulaya linaendelea kutafuta haki kwa ajili ya ndugu na dada zetu nchini Urusi. Tukisubiria hayo, undugu wetu wa ulimwenguni pote unaendelea kuimarishwa na ripoti tunazopata kwa ukawaida katika jw.org, kuhusu imani, ujasiri, na furaha ambayo ndugu zetu nchini Urusi wanayo kwa msaada wa Yehova. —Wafilipi 1:12-14.
a Ona fungu la tatu na la tano la H46-33 Jehovah’s Witnesses of Moscow and Others (Application No. 302/02) and Krupko and Others (Application No. 26587/07) v. Russian Federation.
b Ona fungu la nne la H46-33 Jehovah’s Witnesses of Moscow and Others (Application No. 302/02) and Krupko and Others (Application No. 26587/07) v. Russian Federation.