Hamia kwenye habari

Dada Yekaterina Pegasheva

APRILI 8, 2021
URUSI

Dada Yekaterina Pegasheva Anaendelea Kuwa Mwaminifu Licha ya Kushtakiwa Kuwa Mhalifu Nchini Urusi

Dada Yekaterina Pegasheva Anaendelea Kuwa Mwaminifu Licha ya Kushtakiwa Kuwa Mhalifu Nchini Urusi

HABARI ZA KARIBUNI | Mahakama ya Urusi Yamhukumu Dada Yekaterina Pegasheva Kifungo cha Nje

Mei 31, 2021, Mahakama ya Wilaya ya Gornomariyskiy ya Jamhuri ya Mari El imemhukumu Dada Yekaterina Pegasheva kifungo cha nje cha miaka sita na miezi sita. Hatahitaji kwenda mahakamani wakati huu.

Hukumu Inatarajiwa

Mahakama ya Wilaya ya Gornomariyskiy ya Jamhuri ya Mari El itatangaza hivi karibuni a uamuzi wake katika kesi ya Dada Yekaterina Pegasheva.

Maelezo Mafupi Kumhusu

Yekaterina Pegasheva

  • Alizaliwa: 1989 (Gaintsy, Eneo la Kirov)

  • Maisha Yake: Alizaliwa peke yake katika familia yao. Anapenda kusoma vitabu, kuandika mashairi, na kuimba nyimbo. Anafanya kazi za kutunza nyumba. Alijifunza lugha ya Mari ili kupanua huduma yake

Historia ya Kesi

Oktoba 3, 2019, Dada Pegasheva alikamatwa katika jiji la Yoshkar-Ola, mji mkuu wa Jamhuri ya Mari El. Maofisa walipekua nyumba yake na kuchukua vitabu, vifaa vya kielektroni, barua, na hati zake. Yekaterina alishtakiwa kwa kushiriki utendaji wa shirika lililopigwa marufuku kwa sababu alikuwa akizungumzia habari za Biblia na ndugu na dada zake.

Yekaterina anasema hivi: “Ghafla, maofisa walinitoa nje na kunisukuma kwenye mti wakiwa wameshika mikono yangu nyuma yangu. Nilisali upesi kama Nehemia na kumwomba Yehova msaada.” Baada ya kukamatwa aliwekwa mahabusu kwa zaidi ya siku 100. Sasa yuko chini ya kifungo cha nyumbani.

Yekaterina alihojiwa mara kadhaa alipokuwa mahabusu. Alitambua kwamba mambo aliyojifunza katika Biblia yalimsaidia sana. Anasema hivi: “Nilikumbuka mazoezi na migawo niliyopata nilipohudhuria Shule ya Waeneza-Injili wa Ufalme. Wazo moja hasa liliniimarisha: Unapowajibu maadui wanaokuhoji, unasimama pia mbele ya Bwana Yesu. Hilo lilinisaidia kujizuia na kuwaheshimu wenye mamlaka waliokuwa wakinishtaki isivyo haki.”

Hali imekuwa ngumu kwa kipindi ambacho Yekaterina amewekwa mahabusu na kuwa katika kifungo cha nyumbani. Afya yake imezorota na hawezi kufanya kazi ya kimwili. Ameathiriwa sana kwa sababu ya kutenganishwa na mama na nyanya yake. Licha ya hali hizo ngumu, Yekaterina ameazimia kuendelea kuwa mwaminifu. Anasema hivi: “Kadiri wanavyonishinikiza, ndiyo ninavyoendelea kuvaa mavazi ya silaha kutoka kwa Mungu.” Anaongezea hivi: “Sasa, siogopi jambo lolote! Mwanzoni nilikuwa jasiri, lakini sasa kwa msaada wa roho ya Mungu, nimekuwa jasiri hata zaidi.”

Yekaterina anapoendelea kusubiri uamuzi wa kesi yake, tunajua kwamba ataendelea kumtegemea Yehova, ambaye huwaimarisha watumishi wake wote.—Kutoka 15:2.

a Tarehe ya hukumu haitolewi mapema pindi zote.