MEI 17, 2019
URUSI
Dennis Christensen Atarajia Kujitetea kwa Mara ya Mwisho Mahakamani Mei 23
Siku ya Alhamisi, Mei 16, 2019, kesi ya rufani ya Dennis Christensen ilifanyika kama ilivyopangwa. Viongozi wa mashtaka na mawakili watetezi waliwasilisha hoja zao za kumalizia, na Dennis alipata nafasi ya kujitetea kwa karibu saa nzima. Mabalozi wa kigeni na waandishi wa habari walihudhuria tena—ni jambo linalotia moyo kwamba licha ya kwamba miaka miwili imepita tangu Dennis afungwe na kutangazwa na vyombo vya habari ulimwenguni pote, bado habari kumhusu zinafuatiliwa kwa ukaribu na jumuiya ya kimataifa.
Mwanzoni, kesi yake ilipangwa kusikilizwa hadi siku ya Ijumaa Mei 17. Hata hivyo, mahakimu walitangaza kwamba ingeahirishwa hadi Alhamisi, Mei 23 saa nne asubuhi. Hivyo, Dennis atapata fursa ya mwisho ya kuwasihi mahakimu wamwachilie huru. Ni vigumu kutabiri ikiwa uamuzi utatolewa ifikapo jioni ya Mei 23, au ikiwa mahakama itapanga siku nyingine ya kutangaza uamuzi huo.
Tunajipa ujasiri tunapowaona ndugu zetu kama Dennis Christensen na Sergey Skrynnikov, wakidumisha mtazamo mzuri na kuonyesha tamaa yao ya kubaki waaminifu. Tunahisi kujivunia Mashahidi wenzetu walio nchini Urusi kama Paulo alivyohisi kuhusu Wathesalonike alipoongozwa na roho kuandika maneno haya: “Tunajivunia ninyi kati ya makutaniko ya Mungu kwa sababu ya uvumilivu na imani yenu katika mateso yenu yote na taabu mnayopata.”—2 Wathesalonike 1:4.