Hamia kwenye habari

Kuanzia kushoto kwenda kulia: Ndugu na Dada Sergey na Anna Melnik, Valeriy na Marina Rogozin, na Igor na Yevgeniya Yegozaryan

FEBRUARI 26, 2021
URUSI

HABARI ZA KARIBUNI | Baada ya Miezi Saba Mahabusu, Ndugu Watatu Wanasubiri Hukumu

HABARI ZA KARIBUNI | Baada ya Miezi Saba Mahabusu, Ndugu Watatu Wanasubiri Hukumu

Machi 18, 2022, Mahakama ya Eneo la Volgograd ilikataa ombi la rufaa la Ndugu Sergey Melnik, Valeriy Rogozin, and Igor Yegozaryan. Ndugu wote watatu bado wako gerezani.

Septemba 23, 2021, Mahakama ya Wilaya ya Volgograd Traktorozavodsky iliwahukumu ndugu wote watatu. Ndugu Yegozaryan na Ndugu Melnik walihukumiwa kifungo chao miaka sita gerezani. Ndugu Rogozin alihukumiwa kifungo cha miaka sita na miezi mitano gerezani.

Maelezo Mafupi Kuwahusu

Sergey Melnik

  • Alizaliwa: 1972 (Volgograd, Eneo la Volgograd)

  • Maisha Yake: Alihitimu chuo cha ufundi na kuwa fundi wa magari. Kwa sasa, yeye ni fundi wa paa za nyumba. Alifunga ndoa na Anna mwaka wa 1993. Wana watoto wa kiume watatu. Wanapenda kupanda milima na kufurahia mazingira wakiwa familia

    Anna alianza kujifunza Biblia na Mashahidi wa Yehova. Sergey alipoona mabadiliko aliyofanya, alianza pia kujifunza. Alibatizwa mwaka wa 1999

Valeriy Rogozin

  • Alizaliwa: 1962 (Krasnokamsk, Eneo la Perm)

  • Maisha Yake: Alifanya kazi akiwa rubani katika jeshi kabla ya kustaafu na kuanza kufanya kazi akiwa mhandisi. Alifunga ndoa na Marina mwaka wa 1984. Wana watoto wawili wa kiume

    Alianza kujifunza Biblia katika miaka ya 1990. Alibatizwa mwaka wa 1998

Igor Yegozaryan

  • Alizaliwa: 1965 (Volgograd, Eneo la Volgograd)

  • Maisha Yake: Anafanya kazi ya kutengeneza viatu na vifaa vya umeme. Tangu alipokuwa mtoto alipenda sana muziki. Anajua kupiga gitaa. Alifunga ndoa na Yevgeniya mwaka wa 2002. Wana mtoto mmoja wa kiume

    Alihubiriwa habari njema za Ufalme wa Mungu na mama yake. Alivutiwa sana na jinsi ambavyo kweli za Biblia zinapatana na zinaeleweka. Alibatizwa mwaka wa 1992

Historia ya Kesi

Mei 16, 2019, polisi na Maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa (FSB) walivamia nyumba saba katika Eneo la Volgograd nchini Urusi. Siku mbili baadaye, hakimu wa mahakama kuu ya wilaya aliagiza Ndugu Melnik, Ndugu Rogozin, na Ndugu Yegozaryan wapelekwe mahabusu. Ndugu hao watatu walikaa mahabusu kwa miezi saba.

Ingawa ndugu hao wameruhusiwa kurudi nyumbani, wanakabili changamoto mbalimbali wanaposubiri hukumu. Kwa mfano, Valeriy amewekwa kwenye orodha ya Shirika la Usimamizi wa Fedha la Shirikisho la Urusi. Valeriy anasema hivi: “Akaunti zangu zote za benki zimezuiwa na nimepigwa marufuku kutumia simu na Intaneti. Nilipoteza kazi yangu kwa sababu mimi hutumia simu na Intaneti kufanya kazi.” Yeye na mke wake wamelazimika kutumia pesa za kustaafu ili kujiruzuku. Wamelazimika kurahisisha sana maisha yao.

Sergey na Igor wamewekewa vizuizi na mahakama vinavyofanya iwe vigumu kwao kupata kazi. Sergey anasema kwamba ratiba yake ya kazi inavurgwa sana anapohitaji kwenda mahakamani ili kusikiliza kesi yake. Anasema hivi: “Mimi hufanya kazi ya kutengeneza paa za nyumba, hata hivyo, hivi karibuni nimelazimika kutafuta kazi ndogondogo ninazoweza kumaliza kabla ya kwenda mahakamani.”

Igor ana tatizo la afya linalomlazimu kwenda hospitali mara kwa mara. Anasema hivi: “Kwa sababu ya mashtaka hayo dhidi yangu ni vigumu sana kupata kazi.” Licha ya ugonjwa na matatizo ya kifedha, anaendelea kusema hivi: “Yehova ametupatia zawadi kubwa ya familia ya kiroho ambayo imekuwa pamoja nasi katika nyakati hizi ngumu.”

Ni wazi kwamba ndugu zetu na familia zao wana uhitaji mkubwa wa kimwili kwa sababu ya vizuizi walivyowekewa. Tuna uhakika kwamba ndugu na dada zetu wote nchini Urusi wataendelea kusimama imara licha ya majaribu, wakijua kwamba Yehova ataendelea kuwaandalia mahitaji yao.​—Mathayo 6:33.