NOVEMBA 17, 2020 | HABARI ZILIONGEZWA: FEBRUARI 1, 2023
URUSI
HABARI ZA KARIBUNI—HUKUMU NYINGINE YATOLEWA | Mahakama ya Urusi Yakataa Rufaa ya Mashahidi Watatu
Januari 31, 2023, Mahakama ya Eneo la Kamchatka iliamua kwamba Ndugu Konstantin, na mke wake, Snezhana, pamoja na Dada Vera watatumikia kifungo cha nje cha miaka miwili walichokuwa wamepewa awali. Hawahitaji kwenda gerezani wakati huu.
Desemba 15, 2022, Kamati ya Hukumu ya Kesi za Uhalifu katika Mahakama Kuu ya Urusi ilibadili uamuzi wa kumwondolea mashtaka Ndugu Konstantin Bazhenov, mke wake, Snezhana, na Dada Vera Zolotova. Sasa kesi yao itarudishwa kwenye mahakama ya rufaa. Wawakilishi wa ubalozi sita wa kigeni walihudhuria kesi hiyo ili kuwaunga mkono Mashahidi wa Yehova.
Juni 10, 2022, Mahakama ya Tisa ya Kuchunguza Upya Maamuzi ya Mahakama za Chini ilipinga ombi la mwendesha mashtaka la kubadili uamuzi wa kuwaondolea mashtaka Konstantin, Snezhana, na Vera. Mwendesha mashtaka alikata rufaa kwenye Mahakama Kuu ya Urusi.
Januari 18, 2022, Mahakama ya Eneo la Kamchatka iliunga mkono ombi la pili la rufaa ya Konstantin, mke wake, Snezhana, na Vera. Waliondolewa mashtaka yote mara moja. Mashahidi wote watatu sasa wana haki ya kudai fidia ya kuhukumiwa isivyo haki kama wahalifu. Mwendesha mashtaka atakata rufaa uamuzi huo.
Novemba 17, 2020, Mahakama ya Eneo la Kamchatka ilikataa rufaa katika kesi dhidi ya Konstantin, mke wake, Snezhana, na Vera. Hukumu waliyokuwa wamepewa awali ya miaka miwili katika kifungo cha nje itaanza kutumika sasa. Hawatahitaji kwenda gerezani kwa sasa. Wote watatu wamedumisha shangwe na uthabiti wao.
Septemba 25, 2020, uamuzi ulipokuwa karibu kutolewa, Ndugu Bazhenov alimwambia hakimu kwa ujasiri kwamba haogopi kufungwa. Pia alisema kwamba lilikuwa pendeleo kuwa sehemu ya utimizo wa Yohana 15:20, ambapo Yesu alitabiri kwamba wanafunzi wake wangeteswa.
Ndugu Bazhenov aliikumbusha mahakama kwamba kwenye Mathayo 28:19, 20 Yesu aliwaamuru wanafunzi wake wakahubiri. Kisha Ndugu Bazhenov akauliza swali hili: “Ni nani aliye na haki ya kufuta au kuzuia kile ambacho Kristo ameamuru?” Kisha akasema: “Sitaweza kunyamaza. . . . Nitaendelea kusema kuhusu habari njema kutoka katika Biblia.”