Hamia kwenye habari

Ndugu Yevgeniy Yegorov

APRILI 1, 2021| HABARI ZILIONGEZWA: FEBRUARI 17, 2023
URUSI

HABARI ZA KARIBUNI—NDUGU AHUKUMIWA | Mahakama ya Urusi Inataka Kumnyang’anya Ndugu Yevgeniy Yegorov Uhuru Wake wa Ibada

HABARI ZA KARIBUNI—NDUGU AHUKUMIWA | Mahakama ya Urusi Inataka Kumnyang’anya Ndugu Yevgeniy Yegorov Uhuru Wake wa Ibada

Februari 17, 2023, Mahakama ya Wilaya ya Birobidzhan iliyo katika Eneo Lililotengewa Wayahudi ilimhukumu Ndugu Yevgeniy Yegorov kifungo cha nje cha miaka miwili na nusu. Hahitaji kwenda gerezani wakati huu.

Oktoba 3, 2022, Mahakama ya Eneo Lililotengewa Wayahudi ilipinga uamuzi uliomhukumu Yevgeniy kuwa na hatia. Ilifanya hivyo baada ya Mahakama ya Tisa ya Kuchunguza Upya Maamuzi ya Mahakama za Chini kuamua kurudisha kesi ya Yevgeniy kwenye Mahakama ya Eneo Lililotengewa Wayahudi kwa ajili ya rufaa ya pili. Sasa kesi yake itapelekwa kwenye Mahakama ya Wilaya ya Birobidzhan iliyo katika Eneo Lililotengewa Wayahudi ili isikilizwe upya.

Novemba 25, 2021, Mahakama iliyo katika Eneo Lililotengewa Wayahudi ilikataa ombi la rufaa ya Ndugu Yevgeniy Yegorov. Hukumu yake ya awali itaendelea kutumika. Hatahitaji kwenda gerezani wakati huu.

Juni 21, 2021, Mahakama ya Wilaya ya Birobidzhan iliyo katika Eneo Lililotengewa Wayahudi ilimhukumu Yevgeniy kifungo cha nje cha miaka miwili na nusu.

Maelezo Mafupi Kumhusu

Yevgeniy Yegorov

  • Alizaliwa: 1991 (Birobidzhan)

  • Maisha Yake: Alilelewa na mama na nyanya yake. Amesomea kazi zinazohusiana na umeme. Anafanya kazi ya kutengeneza kufuli na kurekebisha vitu. Anapenda kusoma na kuandika. Amechapisha kitabu na mkusanyo wa mashairi. Alibatizwa na kuwa Shahidi wa Yehova mnamo 2005. Septemba 2019 alifunga ndoa na Kseniya. Mtoto wao wa kiume alizaliwa mnamo Agosti 2020

Historia ya Kesi

Mei 2018, maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa (FSB) walivamia nyumba katika eneo la Birobidzhan. Muda mfupi kabla ya kufunga ndoa, Yevgeniy alishtakiwa kwa “makosa” ya kuabudu na kusoma Biblia. Aliwekewa vizuizi vya kusafiri. Mama ya Yevgeniy, anayeitwa Larisa Artamonova, alishtakiwa muda mfupi baada ya harusi hiyo. Desemba 2019, kesi ya Yevgeniy ilianza kusikilizwa katika Mahakama ya Wilaya ya Birobidzhan.

Yevgeniy anasema kwamba sasa anahisi yuko karibu zaidi na Yehova. Anasema hivi: “Nilipokabili hali ngumu zaidi, Yehova alinituliza na kunipa ‘nguvu zinazopita zile za kawaida.’”​—2 Wakorintho 4:7.

Licha ya kuwa na msaada wa Yehova, Yevgeniy anatambua kwamba lazima ajitayarishe kiakili, kihisia, na kiroho kwa ajili ya mambo ambayo yatatokea wakati ujao. Anaeleza hivi: “Kwa maoni yangu, jambo kuu ni kuendelea kuimarisha uhusiano wangu na Yehova, hata kuwe na hali zipi.”

Licha ya hali ngumu wanazokabili, tuna uhakika kwamba Yevgeniy and Kseniya, pamoja na ndugu na dada zetu nchini Urusi, wataimarishwa na maneno yaliyoongozwa na roho ya Zaburi 10:17: “Lakini utasikia ombi la wapole, Ee Yehova. Utaiimarisha mioyo yao na kuwasikiliza kwa makini.”