Hamia kwenye habari

Kutoka kushoto hadi kulia: Ndugu Yevgeniy Fedin, Ndugu Artur Severinchik, na Ndugu Timofey Zhukov

JULAI 26, 2022 | HABARI ZIMEONGEZWA: DESEMBA 6, 2023
URUSI

HABARI ZA KARIBUNI—NDUGU WAHUKUMIWA | Yehova Anawaimarisha Akina Ndugu Kuvumilia Vifungo Visivyo vya Haki

HABARI ZA KARIBUNI—NDUGU WAHUKUMIWA | Yehova Anawaimarisha Akina Ndugu Kuvumilia Vifungo Visivyo vya Haki

Desemba 5, 2023, Mahakama ya Jiji la Surgut iliyo katika Eneo Lililotengwa la Khanty-Mansi—Yugra iliwahukumu ndugu 17 pamoja na dada mmoja. Miongoni mwao ni Ndugu Yevgeniy Fedin, Ndugu Artur Severinchik, na Ndugu Timofey Zhukov. Ndugu wote 17 walihukumiwa kifungo cha nje cha kati ya miaka sita na miezi mitatu kufikia kifungo cha miaka saba. Dada yetu alihukumiwa kifungo cha nje cha miaka mitatu na miezi mitatu. Hawahitaji kwenda gerezani wakati huu.

Mfuatano wa Matukio

  1. Februari 15, 2019

    Maofisa wa polisi walifanya msako kwenye nyumba nyingi za Mashahidi wa Yehova jijini Surgut na pia katika majiji yaliyo karibu. Ndugu saba walisema kwamba waliteswa walipokuwa wakihojiwa. Ndugu watatu waliwekwa mahabusu, kutia ndani Yevgeniy Fedin na Artur Severinchik

  2. Machi 7, 2019

    Mahakama ya rufaa iliagiza Artur aachiliwe kutoka mahabusu ambako alikuwa amekaa kwa siku 21

  3. Aprili 11, 2019

    Yevgeniy aliachiliwa kutoka mahabusu baada ya miezi miwili hivi. Mahakama ilimwekea vizuizi vya kusafiri, kuwasiliana na wengine, au kutumia Intaneti

  4. Januari 16, 2020

    Hakimu aliamuru kwamba Ndugu Timofey Zhukov aende kwenye hospitali ya watu wenye matatizo ya kiakili ili kufanyiwa uchunguzi. Wapelelezi walipendekeza hilo kwa sababu walisema huenda ana matatizo ya kiakili ndiyo sababu alikataa kujibu maswali walipomhoji, ingawa ana haki ya kutojibu chini ya kufungu cha 51 cha Katiba ya Shirikisho la Urusi. Kwa sababu hiyo Timofey alikata rufaa

  5. Februari 5, 2020

    Timofey alichukuliwa na polisi alipokuwa anatoka mahakamani. Ingawa kesi ya rufaa ilikuwa haijasikilizwa, maofisa hao walimsafirisha umbali wa kilomita 1,200 hadi kwenye hospitali ya watu wenye matatizo ya kiakili iliyo Yekaterinburg, na alibaki huko kwa siku 14

  6. Machi 5, 2020

    Mahakama ya rufaa iliamua kwamba, maofisa hao walimtendea kinyume na haki kwa kumpeleka kwenye hospitali hiyo

  7. Oktoba 19, 2021

    Mahakama ya rufaa iliagiza kwamba Timofey alipwe fidia kwa kuwekwa mahabusu kinyume na haki

  8. Novemba 12, 2021

    Kesi ilipoanza kusikilizwa, mawakili waliowakilisha washtakiwa waliwasilisha uthibitisho kwamba maofisa wa polisi waliwatendea washtakiwa kinyume cha maadili na pia walivunja sheria. Waliwatesa, walipotosha uthibitisho, na walitumia wataalamu wenye ubaguzi. Washtakiwa waliiomba mahakama irudishe kesi hiyo kwa mwendesha-mashtaka.

  9. Novemba 15, 2021

    Hakimu alikiri kwamba maofisa wa polisi walikiuka sheria walipokuwa wakipeleleza, hata hivyo alikataa kurudisha kesi kwa mwendesha-mashtaka

Maelezo Mafupi Kuwahusu

Tuna uhakika kwamba Yehova ataendelea kuwategemeza Yevgeniy, Artur, Timofey, na ndugu na dada wote ambao ‘wanakaza macho yao juu ya vitu visivyoonekana’ wanapoendelea kuvumilia mateso.​—2 Wakorintho 4:17, 18.