Hamia kwenye habari

Kuanzia kushoto kwenda kulia: Ndugu Ilkham Karimov, Ndugu Konstantin Matrashov, Ndugu Vladimir Myakushin, na Ndugu Aydar Yulmetyev

MEI 19, 2021
URUSI

HABARI ZA KARIBUNI | Ndugu Walio Tatarstan Wanathamini Utegemezo Wenye Upendo wa Yehova Wanapokabiliana na Kesi Mahakamani

HABARI ZA KARIBUNI | Ndugu Walio Tatarstan Wanathamini Utegemezo Wenye Upendo wa Yehova Wanapokabiliana na Kesi Mahakamani

Septemba 2, 2022, Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Tatarstan ilikataa ombi la rufaa la Ndugu Ilkham Karimov, Konstantin Matrashov, Vladimir Myakushin, na Aydar Yulmetyev. Hawahitaji kwenda gerezani wakati huu.

Desemba 16, 2021, Mahakama ya Jiji la Naberezhnye Chelny ya Jamhuri ya Tatarstan iliwahukumu Ilkham, Konstantin, Vladimir, na Aydar. Ilkham na Konstantin walihukumiwa kifungo cha nje cha miezi 30. Vladimir alihukumiwa kifungo cha nje cha miezi 37 na Aydar akahukumiwa kifungo cha nje cha miezi 33.

Maelezo Mafupi Kuwahusu

Ilkham Karimov

  • Alizaliwa: 1981 (Jomboy, Uzbekistan)

  • Maisha Yake: Alizoezwa katika fani ya kubadili muundo wa glasi. Alifanya kazi mbalimbali ili kutegemeza familia yake nchini Uzbekistan. Alihamia Urusi mwaka 2000. Siku moja mwaka wa 2001, alisali kwa Mungu apate msaada. Siku iliyofuata, alikutana na Mashahidi wa Yehova na akaanza kujifunza Biblia. Alibatizwa mwaka wa 2004. Mwaka wa 2012 alifunga ndoa na Yulia

Konstantin Matrashov

  • Alizaliwa: 1988 (Prokopyevsk)

  • Maisha Yake: Baba yake alikufa alipokuwa mtoto. Anafanya kazi akiwa fundi wa magari. Anamtegemeza mama yake ambaye alibatizwa Konstantin alipokuwa na miaka minane. Konstantin alivutiwa na ujumbe wa Biblia kwa sababu una tumaini. Alibatizwa mwaka wa 2018

Vladimir Myakushin

  • Alizaliwa: 1987 (Nizhnekamsk)

  • Maisha Yake: Alihitimu katika shule ya ufundi na ya uhandisi. Anafanya kazi akiwa mhandisi mkuu katika kiwanda cha kuzalisha vifaa vya umeme vya magari. Anathamini hekima inayopatikana katika Biblia na anapenda jinsi inavyopatana na akili na kueleweka vizuri. Alibatizwa mwaka wa 2013. Alifunga ndoa na Svetlana mwaka wa 2017

Aydar Yulmetyev

  • Alizaliwa: 1993 (Nizhnekamsk)

  • Maisha Yake: Alijifunza muziki na ufundi wa magari. Anafanya kazi akiwa fundi wa magari na mfanyabiashara. Alianza kujifunza baada ya kuona jinsi kanuni za Biblia zilivyowasaidia wazazi wake. Alibatizwa mwaka wa 2012. Alifunga ndoa na Albina mwaka wa 2013. Alikataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri yake iliyozoezwa na Biblia. Alifanya utumishi wa kiraia wa badala

Historia ya Kesi

Mei 27, 2018, maofisa wa usalama wa Tatarstan walivamia nyumba za Mashahidi kumi na kuwaweka kizuizini Ndugu Ilkham, Ndugu Konstantin, Ndugu Vladimir, na Ndugu Aydar. Kila mmoja wao alibaki kizuizini kwa zaidi ya siku 160 kabla ya kuachiliwa na kuwekwa kwenye kifungo cha nyumbani.

Ingawa waliondolewa kifungo cha nyumbani, kila mmoja wao aliwekwa katika orodha ya “watu wenye msimamo mkali” nchini Urusi na bado mahakama iliwaamuru wasitoke nje ya eneo wanaloishi. Kwa sababu hiyo hawawezi kutumia akaunti zao za benki na pia imekuwa vigumu kwao kupata kazi.

Aydar anasema hivi anapokumbuka wakati alipokuwa kizuizini: “Nilikumbuka mistari mingi, mingi sana ya Biblia. . . . Yehova alinisaidia kukumbuka mambo mengi ambayo nisingeweza kukumbuka nikiwa peke yangu.”

Konstantin alipowekwa kizuizini kwa mara ya kwanza alikuwa na wasiwasi. Lakini upesi alianza kutafuta fursa za kueleza wengine kuhusu imani yake kama vile walinzi, wafungwa wenzake, polisi, na wasimamizi wa gereza. Anasema hivi: “Kuwekwa kizuizini kulinipa fursa ya kutoa ushahidi zaidi kuliko wakati nilipokuwa huru. Ni kama vile mtume Paulo alivyoandika katika karne ya kwanza kwenye Wafilipi 1:12, 13: ‘Basi ninataka mjue, akina ndugu, kwamba hali yangu kwa kweli imesaidia kuendeleza habari njema, hivi kwamba vifungo vyangu vya gereza kwa ajili ya Kristo vimejulikana wazi kati ya Walinzi wote wa Mfalme na watu wengine wote.’”

Vladmir alithamini jinsi akina ndugu na dada walivyomsaidia. Anasema hivi: “Mke wangu aliniambia kwamba ndugu na dada walimpa pesa alizotumia kununua vitu nilivyohitaji na kunitumia. Kituo cha mahabusu kilikuwa na wastani fulani wa vitu ambavyo ungepokea kila mwezi na mara nyingi nilifikia wastani huo.”

Ilkham alielezea jinsi uhusiano wake na Yehova ulivyoimarika. Alisema: “Kwa sababu ya kesi hii, nimekuwa na uhusiano wa karibu zaidi na Baba yangu wa mbinguni. Ninamtumaini zaidi na ninamtegemea hata zaidi. Sala zangu zimekuwa ndefu zaidi, zenye maana zaidi, na zinatoka moyoni.”

Tunajua kwamba ndugu hawa na familia zao watapata baraka kwa sababu ya “ujitoaji-kimungu kamili na kuchukua mambo kwa uzito” wakati wa majaribu haya.​—1 Timotheo 2:2.