Hamia kwenye habari

Kuanzia kushoto hadi kulia: Ndugu Arsen Avanesov, Vilen Avanesov, na Aleksandr Parkov

MEI 12, 2021
URUSI

HABARI ZA KARIBUNI | Ndugu Watatu Wawekwa Mahabusu kwa Muda Mrefu

HABARI ZA KARIBUNI | Ndugu Watatu Wawekwa Mahabusu kwa Muda Mrefu

Juni 23, 2022, Mahakama ya Nne ya Kuchunguza Upya Maamuzi ya Mahakama za Chini ilikataa kwa mara ya pili rufaa ya Ndugu Vilen Avanesov na Ndugu Aleksandr Parkov. Kulingana na maombi ya mwendesha-mashtaka, mahakama ilirudisha kesi dhidi ya Ndugu Arsen Avanesov kwenye hatua ya kwanza ya rufaa. Kwa sababu hiyo, huenda Ndugu Arsen akapata hukumu kali zaidi. Ndugu wote watatu bado wapo gerezani.

Decemba 6, 2021, Mahakama ya Eneo la Rostov ilikataa rufaa ya Arsen, Vilen, na Aleksandr. Hivyo wamebaki gerezani.

Julai 29, 2021, Mahakama ya Wilaya ya Leninskiy ya Rostov-on-Don ilitoa hukumu ya miaka sita na nusu gerezani dhidi ya Ndugu Arsen na Ndugu Aleksandr na hjukumu ya miaka sita dhidi ya Ndugu Vilen. Ndugu wote watatu tayari wametumikia zaidi ya miaka miwili wakiwa mahabusu na hivyo watabaki gerezani wakati huu

Maelezo Mafupi Kuwahusu

Arsen Avanesov

  • Alizaliwa: 1983 (Baku, Azerbaijan)

  • Maisha Yake: Alisomea ufundi na akafanya kazi ya ujenzi. Alipokuwa kijana alipenda kucheza mpira wa raga. Alijifunza Kiingereza na Kifaransa

    Kwa msaada wa wazazi wake, alisitawisha uthamini kwa ajili ya Biblia. Alibatizwa na kuwa Shahidi wa Yehova katika mwaka wa 2005

Vilen Avanesov

  • Alizaliwa: 1952 (Baku, Azerbaijan)

  • Maisha Yake: Alifanya kazi akiwa fundi umeme na mjenzi. Anafurahia kupika, kuoka mikate, na kusoma. Biblia ilikuwa mojawapo ya vitabu alivyopenda zaidi alipokuwa kijana

    Alifunga ndoa na Stella, katika mwaka wa 1980. Wana mwana mmoja anayeitwa Arsen, na binti anayeitwa Elina. Familia yao ilihamia Armenia wakiwa wakimbizi mwaka wa 1988. Mwaka huohuo, familia yao ililazimika kuhama kwa sababu ya tetemeko la ardhi lililotokea Yerevan, Armenia, na pia kwa sababu hali za kiuchumi ziliendelea kuzorota. Walihamia Rostov-on-Don, nchini Urusi. Vilen alibatizwa mwaka wa 2006

Aleksandr Parkov

  • Alizaliwa: 1967 (Spassk, Eneo la Kemerovo)

  • Maisha Yake: Tangu alipokuwa kijana, alijifunza kufanya kazi ngumu kwenye shamba na kuchunga mifugo. Alifanya kazi ya kuendesha trekta na kutengeneza sanaa za shaba

    Alifunga ndoa na Galina mwaka wa 1990. Walianza kujifunza Biblia pamoja. Alibatizwa mwaka wa 1992. Wana binti watatu na wajukuu wawili

Historia ya Kesi

Mei 22, 2019, nyumba kadhaa za Mashahidi wa Yehova zilivamiwa katika eneo la Rostov-on-Don. Ndugu Vilen Avanesov na mwana wake Arsen, pamoja na Ndugu Aleksandr Parkov walikamatwa na wamekuwa mahabusu kwa karibu miaka miwili. Mnamo Machi 2021, ndugu hao watatu waliwekwa kizuizini katika eneo lingine.

Stella, mke wa Vilen hajaruhusiwa kumwona mume wake na mwana wake. Pia, ameachwa bila njia ya kupata riziki. Galina, mke wa Aleksandr, alifunguliwa kesi pia kwa sababu ya imani yake. Mahakama ilimhukumu na kumpa kifungo cha nje cha miaka miwili na miezi mitatu.

Undugu wa ulimwenguni pote umehuzunishwa sana na jinsi ndugu zetu walivyokamatwa bila haki. Sote tutaendelea ‘kuwakumbuka wale walio gerezani, kana kwamba tumefungwa pamoja nao.’—Waebrania 13:3.