Hamia kwenye habari

Kuanzia kushoto hadi kulia, safu ya juu: Ndugu Yuriy Geraskov, Maksim Khalturin, Vladimir Korobeynikov, na Andrzej Oniszczuk. Safu ya chini: Ndugu Andrey Suvorkov, Yevgeniy Suvorkov, na Vladimir Vasilyev

APRILI 22, 2021
URUSI

HABARI ZA KARIBUNI—RUFAA YAKATALIWA | Sala, Kujifunza, na Kitia-moyo cha Kiroho Kiliwasaidia Akina Ndugu Kuvumilia Muda Waliokuwa Mahabusu na Kifungo cha Nyumbani

HABARI ZA KARIBUNI—RUFAA YAKATALIWA | Sala, Kujifunza, na Kitia-moyo cha Kiroho Kiliwasaidia Akina Ndugu Kuvumilia Muda Waliokuwa Mahabusu na Kifungo cha Nyumbani

Oktoba 4, 2022, Mahakama ya Eneo la Kirov ilikataa ombi la rufaa la Ndugu Maksim Khalturin, Vladimir Korobeynikov, Andrzej Oniszczuk, Andrey Suvorkov, Yevgeniy Suvorkov, na Vladimir Vasilyev. Hawahitaji kwenda gerezani wakati huu.

Juni 3, 2022, Mahakama ya Wilaya ya Pervomayskiy ya Kirov iliwahukumu Ndugu Maksim Khalturin, Vladimir Korobeynikov, Andrzej Oniszczuk, Andrey Suvorkov, Yevgeniy Suvorkov, na Vladimir Vasilyev kifungo cha nje cha kati ya miaka miwili na nusu hadi miaka sita na nusu. Mahakama ilisema kwamba Ndugu Yuriy Geraskov alikuwa na hatia licha ya kwamba alikufa kabla ya kesi hiyo kwisha.

Maelezo Mafupi Kuwahusu

Yuriy Geraskov

  • Alizaliwa: 1956 (Azerbaijan)

  • Alikufa: Aprili 24, 2020

  • Maisha Yake: Tangu alipokuwa mtoto alipenda kucheza mpira na kupiga picha. Alifanya kazi kwenye okestra. Alihamia Urusi mnamo 1993 kwa sababu ya hali ya kisiasa nchini Azerbaijan. Alifunga ndoa na Alevtina katika mwaka wa 2011. Mwaka huohuo alibatizwa na kuwa Shahidi wa Yehova. Wenzi hao wa ndoa walipenda kwenda matembezi na kuwatembelea marafiki

Maksim Khalturin

  • Alizaliwa: 1974 (Kirov, Eneo la Kirov)

  • Maisha Yake: Alipokuwa mtoto alisitawisha hamu ya kusoma. Alipendezwa kusoma Biblia kwa mara ya kwanza mnamo 1993. Alibatizwa na kuwa Shahidi wa Yehova katika mwaka wa 1995. Anawatunza wazazi wake wenye umri mkubwa. Wanaunga mkono imani yake ya kidini ingawa wao ni wa dini tofauti

Vladimir Korobeynikov

  • Alizaliwa: 1952 (Kisiwa cha Dikson, Eneo la Krasnoyarsk)

  • Maisha Yake: Baba yake alikuwa mchunguzi wa bahari kwenye ncha ya dunia. Alipokuwa mtoto, Vladimir alipenda kutengeneza vigezo vya vitu. Alifanya kazi akiwa fundi-bomba na kurekebisha mashine. Sasa amestaafu na anapenda kuvua samaki

    Yeye na mke wake, Olga, walianza kujifunza Biblia na Mashahidi wa Yehova mapema katika miaka ya 1990. Alipendezwa hasa na unabii wa Biblia. Alibatizwa mnamo 1996. Kanuni za Biblia ziliimarisha familia yao, yenye mwana na binti ambao ni watu wazima

Andrzej Oniszczuk

  • Alizaliwa: 1968 (Białystok, Poland)

  • Maisha Yake: Alipenda kucheza mpira na kuinua vyuma alipokuwa kijana. Alibatizwa katika mwaka wa 1990. Alihamia Kirov mwaka wa 1997. Anapenda vitabu vya Kirusi. Alifunga ndoa na Anna mnamo mwaka wa 2002. Wanapenda kwenda matembezi nje, wakikusanya uyoga, na kucheza mpira

Andrey Suvorkov

  • Alizaliwa: 1993 (Kirov)

  • Maisha Yake: Mama yake alimfundisha kweli tangu alipokuwa mtoto mchanga. Alipokuwa mtoto, alipenda kujifunza sayansi na kucheza michezo, hasa mpira wa wavu. Alibatizwa na kuwa Shahidi wa Yehova mnamo 2007. Alipewa kazi katika kituo cha kuwatibu watu walioathiriwa na dawa za kulevya badala ya kwenda jeshini. Alifunga ndoa na Svetlana katika mwaka wa 2016. Wanapenda kucheza michezo

Yevgeniy Suvorkov

  • Alizaliwa: 1978 (Kumeny, Eneo la Kirov)

  • Maisha Yake: Alipokuwa mtoto, alipenda kucheza chesi, mpira wa magongo, na kusikiliza muziki. Anafanya kazi akiwa fundi-umeme. Alianza kujifunza Biblia na Mashahidi wa Yehova alipokuwa na umri wa miaka 16. Alibatizwa mnamo 1995. Aliomba kufanya utumishi wa badala wa kijeshi alipokuwa na umri wa miaka 18. Hatimaye alipewa utumishi wa kiraia baada ya kuomba mara sita. Alifunga ndoa na Svetlana mwaka wa 2000 na kumsaidia kulea mwana wake, Andrey (aliyetajwa juu)

Vladimir Vasilyev

  • Alizaliwa: 1956 (Perm)

  • Maisha Yake: Alipenda kucheza mpira alipokuwa mtoto. Alifanya kazi akiwa fundi bomba na dereva. Sasa amestaafu. Yeye na mke wake Nadezhda, walianza kujifunza Biblia na Mashahidi wa Yehova mwanzoni mwa miaka ya 1990. Alibatizwa katika mwaka wa 1994

Historia ya Kesi

Oktoba 9, 2018, wenye mamlaka walifanya upekuzi katika nyumba 14 za Mashahidi wa Yehova katika eneo la Kirov. Kwa sababu hiyo, Ndugu Maksim Khalturin, Ndugu Vladimir Korobeynikov, Ndugu Andrzej Oniszczuk, Ndugu Andrey Suvorkov, na Ndugu Yevgeniy Suvorkov walikamatwa. Baada ya hapo waliwekwa mahabusu. Katika mwezi wa Januari na Julai 2019, Ndugu Vladimir Vasilyev na Ndugu Yuriy Geraskov walishtakiwa pia.

Vladimir Korobeynikov aliwekwa kizuizini kwa zaidi ya miezi miwili. Aliachiliwa na kuwekwa katika kifungo cha nyumbani ili aweze kumtunza mke wake aliyekuwa mgonjwa na pia binti yake. Maksim na Andrey waliwekwa kizuizini kwa zaidi ya miezi mitatu. Yevgeniy aliwekwa humo kwa miezi mitano hivi. Andrzej aliwekwa kizuizini kwa siku 327. Baadhi ya ndugu hawa walihamishiwa kwenye kifungo cha nyumbani. Kwa sasa wameachiliwa lakini hawaruhusiwi kusafiri nje ya eneo lao.

Walipokuwa kizuizini, walikabili changamoto ya kutenganishwa na familia zao. Lakini walikuwa na uhakika kamba Yehova angewatunza wapendwa wao.

Kwa mfano, Olga, mke wa Vladimir Korobeynikov, ni mlemavu. Anasema hivi: “Jambo gumu zaidi lilikuwa kutambua kwamba nilikuwa nimemwacha mke wangu asiyejiweza nyumbani akiwa peke yake.” Anaongezea kueleza kwamba wakati wa uvamizi simu ya mke wake ilichukuliwa. Jambo hilo lilimhangaisha sana Vladimir hadi alipopata barua kutoka dada mmoja wa kiroho aliyemhakikishia kwamba Wakristo wenzake walikuwa wakimtunza mke wake. Baadaye Olga alimtumia barua yenye kufariji sana iliyomhakikishia kwamba yuko sawa.

Kuwekewa vizuizi vya kusafiri na kuwekwa katika orodha ya watu wanaoonwa kuwa “wenye msimamo mkali” kumewaletea matatizo zaidi. Kwa mfano, si rahisi kwa ndugu hao kupata kazi za kudumu. Isitoshe, hawawezi kutumia akaunti zao za benki.

Hata hivyo, Yevgeniy anasema hivi: “Yehova hutuandalia mahitaji yetu yote kwa wingi. Kama Waisraeli nyikani, hatukosi lolote. Tunajionea kikamili jinsi watu katika familia ya Yehova wanavyotunzana kimwili, kihisia, na kiroho.”

Ndugu hao wanasema kwamba sala, funzo la kibinafsi, na kusoma Biblia kumewasaidia kuendelea kuwa imara na jasiri. Kwa mfano, Vladimir Vasilyev anaeleza hivi: “Matukio yanayofafanuliwa katika Biblia yanatusaidia kuelewa kwamba Yehova ana uwezo wa kudhibiti kila kitu. Kwa sababu hiyo, imani yetu katika Mungu imeimarishwa, na bila shaka, uhakika wetu kwake unazidi kuongezeka.”

Ingawa kesi yao imewaletea ndugu hao na familia zao matatizo, tunajua kwamba wataendelea kumtegemea Yehova. Wanaendelea kuvumilia wakijua kwamba “mwanadamu ambaye ni duni tu” hawezi kutokeza madhara ya kudumu.​—Zaburi 56:4.