Hamia kwenye habari

OKTOBA 14, 2019
URUSI

Hati Yenye Maneno ya Kumalizia ya Ndugu Valeriy Moskalenko

Hati Yenye Maneno ya Kumalizia ya Ndugu Valeriy Moskalenko

Ijumaa, Agosti 30, 2019, Ndugu  Valeriy Moskalenko alitoa maneno yake ya kumalizia mahakamani. Ifuatayo ni sehemu ya hati (imetafsiriwa kutoka katika lugha ya Kirusi) ya maelezo yake:

Mheshimiwa Hakimu na wengine waliohudhuria, nina umri wa miaka 52 na mwaka uliopita niliwekwa chini ya ulinzi. Umekuwa mwaka mmoja kamili sasa.

Katika maneno yangu ya mwisho kwenye mahakama hii, ningependa kuwaambia kwa kifupi mambo fulani kuhusu mimi, na jinsi ninavyoona shtaka langu la uhalifu, na kuhusu maoni yangu binafsi ya uhai. Ninatumaini kwamba wewe, Mheshimiwa, utaelewa kwa nini sitakana imani yangu kwa Mungu na kwa nini kuwa na imani kwa Mungu si kosa.

Sikuzaliwa nikiwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova. Wazazi wangu walikuwa watu wema na walinilea vizuri, lakini hata nilipokuwa ningali mtoto nilisumbuka sana kujua kwamba kulikuwa na ukosefu wa haki kila mahali. Niliwaza hivi, ‘Mambo hayapaswi kuwa hivi—watu waovu na wadanganyifu wanazidi kuongezeka, na watu wanyoofu na wenye fadhili wanateseka.’

Nikiwa na umri wa miaka 24, nilipata majibu ya maswali yangu baada ya kufanya utafiti wa kina na kujifunza Biblia kwa miezi kadhaa.

Toka wakati huo nimekuwa nikijaribu kufanya maamuzi yanayozingatia hisia, sheria na kanuni za Mungu ambazo zinaonyeshwa kwa kina [katika Biblia] na kuonekana katika maisha ya [waabudu] wa Yehova walioishi zamani.

Ninaishi na mama yangu. Amezeeka na anahitaji msaada wangu. Mnamo Agosti 1, 2018, mama yangu alipokuwa nyumbani peke yake, maofisa kutoka Idara ya Kimataifa ya Usalama (FSB), waliagiza Kikosi Maalumu kukata mlango wangu kwa kutumia msumeno. Hii ndiyo njia ambayo wapelelezi waliamua kuingia ndani ya nyumba yangu ili kufanya msako.

Mama yangu alishtuka sana. Baada ya kikosi hicho cha polisi waliofunika nyuso kuvamia nyumba yetu, mama alipata mshtuko wa moyo hivyo gari la wagonjwa likaitwa. Nilipojua kwamba polisi walikuwa nyumbani kwangu, nilifika baada ya dakika 30. Nilipoona hali ya mama yangu, shinikizo langu la damu lilipanda. Licha ya haya yote, sikukasirika na nilijaribu kuendelea kuwa mtulivu. Nilikuwa na fadhili—kama inavyompasa Mkristo. Mungu wangu, Yehova, amenifundisha sifa hiyo na sitaki kumkasirisha.

Samahani sana Mheshimiwa, kwa kawaida huwa sijizungumzii sana. Hii si tabia yangu, lakini sasa ninalazimika kufanya hivyo.

Nimekuwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova kwa zaidi ya miaka 25 sasa. Hiyo ni sehemu kubwa ya maisha yangu. Na muda wote huo sijawahi kudhaniwa kuwa mtu mwenye msimamo mkali. Tofauti kabisa na hilo, nimejulikana kama jirani mwema, mfanyakazi mwenye bidii, na mtoto mwenye kujali.

Ghafla, tokea Aprili 20, 2017, nimekuwa nikiitwa mtu mwenye msimamo mkali. Kwa vigezo gani? Nini kimebadilika? Je, nimekuwa mtu mbaya? Hapana. Je, nimekuwa mtu mkatili au nimemsababishia mtu yeyote maumivu au mateso yoyote? Hapana. Je, nimepoteza haki ya kutumia Kifungu cha 28 cha Katiba ya Urusi? Hapana. Jina langu halikuorodheshwa katika uamuzi wa Mahakama Kuu. Hakuna mtu aliyenizuia haki yangu ya kutumia Katiba ya Shirikisho la Urusi, hususa ni Kifungu cha 28. Hivyo basi, kwa nini niko hapa katika kiti cha mshtakiwa?

Kulingana na mazungumzo yangu na mpelelezi, ilionekana wazi zaidi kwamba nilikamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi kwa sababu mimi ni mwamini anayetumia jina la Mungu Mwenye Enzi Kuu, Yehova katika sala na mazungumzo yangu. Lakini hili si kosa. Mungu mwenyewe amajichagulia jina lake na kuhakikisha kwamba linarekodiwa katika Biblia.

Ninarudia tena na tena kwamba ni jambo lisilowaziwa kwa mimi kutenda kinyume na mapenzi ya Mungu yanayoonyeshwa waziwazi katika Biblia. Na haitajalisha jinsi nitakavyoshinikizwa au kuadhibiwa—hata ikiwa nitahukumiwa kifo—ninatangaza kwamba sitamwacha Muumba Mweza-Yote, Yehova Mungu.

Mheshimiwa, Mashahidi wa Yehova wanajulikana ulimwenguni pote kuwa watu wenye urafiki na wapenda-amani. Haki zao kama waamini zinaheshimiwa na nchi nyingi zaidi duniani. Ningependa sana kwamba haki za waamini ziheshimiwe nchini Urusi pia, na katika hali yangu, ziheshimiwe nikiwa kama mwamini pia.

Sina hatia ya kosa ninaloshtakiwa na ninaomba mahakama itoe uamuzi wa kwamba sina hatia!

Asante!