AGOSTI 7, 2019
URUSI
Idadi ya Nyumba za Mashahidi wa Yehova Zilizovamiwa na Askari Nchini Urusi Yafikia 600
Katika kipindi cha miezi 18 iliyopita, polisi na maofisa wa usalama wa FSB (Federal Security Service) huko Urusi wamevamia jumla ya nyumba 613 za ndugu na dada zetu. Tangu Januari 2019, askari wamevamia nyumba 332. Idadi hiyo inazidi nyumba zilizovamiwa mwaka wa 2018, yaani 281.
Serikali imeongeza mashambulizi dhidi ya ndugu na dada zetu katika miezi ya hivi karibuni. Mwezi wa Juni nyumba 71 zilivamiwa, na mwezi wa Julai nyumba 68 zilivamiwa—hilo lilikuwa ongezeko kubwa zaidi kwa kulinganisha na wastani wa nyumba 23.4 zilizovamiwa kila mwezi mwaka wa 2018.
Kwa kawaida, wakati wa uvamizi kikundi cha askari waliofunika nyuso zao na walio na silaha hukusanyika nje ya nyumba. Baada ya kuingia ndani ya nyumba, wakati mwingine askari hao huwatisha Mashahidi kwa bunduki, kutia ndani watoto na waliozeeka, kana kwamba wao ni wahalifu sugu na walio hatari. Hilo linaonyesha sababu inayofanya baadhi ya wataalamu wakubaliane na Dakt. Derek H. Davis, aliyekuwa mkurugenzi wa Chuo Kikuu cha Baylor, Taasisi ya J.M. Dawson ya Mafunzo ya Kanisa na Serikali, aliyesema: “Mashambulizi ya serikali ya Urusi dhidi ya kikundi chenye amani cha Mashahidi wa Yehova ni makali kupita kiasi.”
Inasikitisha kwamba, kadiri mashambulizi hayo yanavyozidi kuongezeka, ndivyo kesi za uhalifu dhidi ya ndugu zetu zinavyozidi kuongezeka. Sasa kuna ndugu na dada 244 wanaokabili mashtaka ya uhalifu nchini Urusi na Krimea. Idadi hiyo imeongezeka maradufu tangu Desemba 2018, ambapo kulikuwa na kesi 110 za uhalifu. Kati ya ndugu na dada 244 wanaokabili mashtaka, 39 wamewekwa kizuizini, 27 wamezuiliwa nyumbani, na zaidi ya 100 are wanakabili vizuizi mbalimbali.
Ingawa ndugu na dada zetu wanaendelea kushambuliwa na serikali ya Urusi, ‘hatutikiswi na dhiki hizi.’ Badala yake, tunatiwa moyo na ripoti kwamba ndugu zetu wanaendelea kuwa washikamanifu na wavumilivu. Tunaendelea kumsifu na kumshukuru Yehova kwa kujibu sala zetu nyingi kwa niaba yao, na tuna hakika kwamba ataendelea kufanya hivyo.—1 Wathesalonike 3:3, 7.