Hamia kwenye habari

Ndugu Vladimir Alushkin kabla ya kukamatwa na kuwekwa kizuizini

NOVEMBA 13, 2019
URUSI

Kamati ya Umoja wa Mataifa Yaagiza Urusi Imwachilie Huru Ndugu Alushkin

Kamati ya Umoja wa Mataifa Yaagiza Urusi Imwachilie Huru Ndugu Alushkin

Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Vifungo Visivyo vya Haki (WGAD) imechapisha ripoti yenye kurasa 12 ikisema kwamba Urusi ilivunja sheria kwa kumkamata na kumfunga Ndugu Vladimir Alushkin. Ripoti hiyo imeagiza kwamba nchi ya Urusi imwachilie Ndugu Alushkin na kumlipa fidia kwa sababu ya kuvunja haki zake.

Ndugu Alushkin alikamatwa Julai 15, 2018, baada ya polisi 12 hivi wenye bunduki na waliofunika nyuso zao kuvunja na kuingia nyumbani kwake. Maofisa walifanya msako katika nyumba yake kwa karibu saa nne, wakachukua simu za mkononi, vifaa vya kielektroni, Biblia, na machapisho mengine kisha wakampeleka kwa maofisa wa upelelezi ili akahojiwe.

Ndugu Vladimir Alushkin kwenye Mahakama ya Wilaya ya Pervomayskiy huko Penza mnamo Januari 2019

Wenye mamlaka walimweka Ndugu Alushkin kizuizini kwa siku mbili kabla Mahakama ya Wilaya ya Pervomayskiy huko Penza kuagiza kwamba awekwe mahabusu kwa miezi miwili. Baada ya hapo mahakama hiyo iliongeza mara mbili muda wa Ndugu Alushkin wa kukaa kizuizini. Baada ya kukaa karibu miezi sita kizuizini, alihamishwa na kupelekwa kwenye kifungo cha nyumbani, kinachoendelea kufikia sasa.

Katika jitihada za kuondolewa mashtaka na kuwekwa huru, Ndugu Alushkin alikata rufaa kwa WGAD. Jopo hilo la wataalamu wa haki za kibinadamu, lililopewa mamlaka na Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za Kibinadamu, hushughulikia maombi ya watu binafsi kuhusu kuzuiliwa na polisi kinyume cha sheria au amri ya mahakama ya kifungo cha nyumbani, kuwekwa kizuizini kabla ya kesi, na kufungwa gerezani.

Baada ya kuchunguza kwa makini shtaka la Urusi kwamba Ndugu Alushkin alijihusisha na shughuli za msimamo mkali, kamati ya WGAD ilisema: “Shughuli zote ambazo Bw. Alushkin alijihusisha nazo zilihusu mazungumzo ya kidini yaliyofanywa kwa amani. Kamati hiyo ilitambua kwamba alichofanya Bw. Alushkin ni kutumia uhuru wake wa kidini kulingana na kifungu cha 18 kwenye Mkataba [Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa, na nchi ya Urusi ni mwanachama wa mkataba huo].” Kwa hiyo, ripoti hiyo ilisema “Kamati hii inasisitiza kwamba Bw. Alushkin hakupaswa kukamatwa na kuwekwa kizuizini na hapaswi kufunguliwa mashtaka yoyote.” Isitoshe, WGAD imeomba serikali ya Urusi “ishughulikie kisa cha Bw. Alushkin bila kukawia,” na kusisitiza kwamba “hatua inayofaa ni kumwachilia huru Bw. Alushkin mara moja.”

WGAD inatambua kwamba kisa cha Ndugu Alushkin ni moja kati ya visa vingi nchini Urusi. Yeye ni “mmoja kati ya idadi inayoongezeka ya Mashahidi wa Yehova katika Muungano wa Urusi ambao wamekamatwa, kuzuiliwa na kushtakiwa kwa shughuli za kihalifu kwa sababu tu ya kutumia haki yao ya uhuru wa kidini”—haki inayolindwa na sheria za kimataifa. Hivyo, ili kupinga mnyanyaso dhidi ya waabudu wenzetu nchini Urusi, WGAD imesema waziwazi kwamba ripoti yao haikuhusu tu kisa cha Ndugu Alushkin bali pia Mashahidi wote wa Yehova wanaokabili “hali kama ya Bw. Alushkin.”

Bado serikali ya Urusi haijachukua hatua ili kutekeleza mapendekezo ya WGAD. Badala yake, Agosti 2019 wenye mamlaka huko Penza nchini Urusi walimfungulia mashtaka Ndugu Alushkin. Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa Novemba 15, 19, na 22, 2019.

Ingawa tunatumaini kwamba mahakama hiyo ya Urusi itazingatia ripoti ya WGAD itakapofanya uamuzi wa mwisho katika kesi ya Ndugu Alushkin, kama mtunga zaburi, tunamtegemea kabisa Yehova: “Sitaogopa. . . . Yehova yuko upande wangu akiwa msaidizi wangu . . . Ni bora kumkimbilia Yehova.”—Zaburi 118:6-9.