MEI 14, 2019
URUSI
Kesi ya Rufaa ya Christensen Yakaribia Kuisha
Jumanne, Mei 7, 2019, Mahakama ya Mkoa wa Oryol, ilianza kusikiliza rufaa ya kesi ya Dennis Christensen ya kupinga hukumu ya kifungo cha miaka sita gerezani aliyohukumiwa kwa kosa la kutenda kupatana na imani yake. Lakini mahakama hii imeendeleza mwenendo wa mahakama za Kirusi za awali, na kukataa kuzingatia kile ambacho mawakili wanaona kuwa ushahidi mkubwa wa kuonyesha kwamba Dennis hana hatia. Hilo jopo la mahakimu watatu linaweza kutangaza uamuzi wake mwishoni mwa juma hili.
Kesi iliposikilizwa kwa mara ya kwanza, ndugu na dada wengi walienda mahakamani ili kumtia moyo Dennis. Hata mabalozi kutoka nchi mbalimbali walihudhuria pamoja na waandishi wa habari na mawakili watetezi wa haki za kibinadamu. Kesi ilianza kusikilizwa katika chumba kidogo ambacho watu 20 hadi 25 tu ndio wangeingia, hivyo watu 50 hivi walibaki nje. Hata hivyo, mahakama ilikubali ombi la mawakili wa Dennis la kuhamia kwenye chumba kikubwa zaidi ambacho kingetoshea watu 80 hivi. Kesi iliacha kusikilizwa baada ya saa tatu.
Kesi iliposikilizwa kwa mara ya pili, mahakimu walikataa ombi la mawakili la kwamba ushahidi wake uchunguzwe tena ili kuthibitisha kwamba hana hatia. Ni jambo linalosikitisha kwa sababu mawakili wa Dennis wanaamini kuwa ushahidi huo ungethibithisha kwamba alihukumiwa kimakosa mwanzoni. Mwishoni mwa siku hiyo, mahakama ilitangaza kwamba kesi itasikilizwa tena Alhamisi, Mei 16, na hoja za mwisho zitawasilishwa.
Tunaendelea kusali kwamba ndugu zetu nchini Urusi wadumishe amani yao na imani thabiti katika ahadi za Yehova kwamba mwishowe atawaokoa kutoka kwa wale wanaowatendea kwa dharau.—Zaburi 12:5.