Hamia kwenye habari

Ndugu Sergey Klimov akiwa kizuizini katika mahakama Mei 2019

NOVEMBA 11, 2019
URUSI

Mahakama Nchini Urusi Yamhukumu Ndugu Klimov Miaka Sita Gerezani, Kifungo Kirefu Zaidi Tangu Marufuku ya Mwaka 2017

Mahakama Nchini Urusi Yamhukumu Ndugu Klimov Miaka Sita Gerezani, Kifungo Kirefu Zaidi Tangu Marufuku ya Mwaka 2017

Novemba 5, 2019, Mahakama ya Wilaya ya Tomsk ya Oktyabrsky ilimhukumu Ndugu Sergey Klimov kifungo cha miaka sita gerezani. Ndugu Dennis Christensen ndiye ndugu pekee nchini Urusi aliyehukumiwa kifungo kirefu hivyo. Hata hivyo, kuhusu Ndugu Klimov, mahakama iliongeza vizuizi vingine, na kufanya kifungo chake kuwa kifungo kirefu zaidi tangu 2017, Mahakama Kuu ilipowapiga marufuku Mashahidi.

Ndugu Klimov alikamatwa tarehe 3 Juni, 2018, baada ya maofisa wa polisi na kikosi maalumu kuvamia nyumba mbili za Mashahidi wa Yehova. Ndugu na dada 30 hivi walikamatwa na kwenda kuhojiwa, kutia ndani dada mwenye umri wa miaka 83. Wote waliachiliwa isipokuwa Ndugu Klimov. Alifunguliwa mashtaka ya kihalifu na mahakama ikaamuru awekwe kizuizini miezi miwili akisubiri kesi ianze. Muda wake wa kukaa kizuizini uliongezwa mara saba, ikimaanisha kwamba hata kabla ya kuanza kifungo chake cha miaka sita, tayari alikuwa amefungwa na kutenganishwa na mke na familia yake kwa mwaka mmoja na miezi mitano.

Mawakili wa Ndugu Klimov watakata rufaa ya uamuzi huo. Pia, Agosti 20, 2018, malalamiko ya Klimov dhidi ya Urusi yaliwasilishwa kwenye Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu kuhusu muda aliokaa kizuizini.

Mwaka wote wa 2019, kumekuwa na ongezeko la uvamizi, kukamatwa kwa ndugu zetu na kuwekwa kizuizini nchini Urusi. Licha ya mambo hayo yote, ndugu zetu hawavunjiki moyo. Tunatiwa moyo na uthibitisho wa wazi kwamba Yehova anawabariki ndugu zetu wanapoendelea kumtegemea kabisa.—Zaburi 56:1-5, 9.