Hamia kwenye habari

Kushoto kwenda kulia: Ndugu Aleksandr Prianikov, Dada Venera Dulova, pamoja na binti yake Dada Darya Dulova, kabla ya kesi yao

JANUARI 24, 2020
URUSI

Mahakama ya Karpinsk, Urusi, Yatarajiwa Kutangaza Ikiwa Ndugu Mmoja na Dada Wawili Wana Hatia ya Kosa la Uhalifu

Mahakama ya Karpinsk, Urusi, Yatarajiwa Kutangaza Ikiwa Ndugu Mmoja na Dada Wawili Wana Hatia ya Kosa la Uhalifu

Jumatatu Januari 27, 2020, Mahakama ya Jiji la Karpinsk inatarajiwa kutangaza uamuzi wake katika kesi inayomhusu Dada Vanera na Darya Dulova pamoja na Ndugu Aleksandr Prianikov. Mwendesha-mashtaka ameomba Ndugu Prianikov na Dada Vanera Dulova wapewe kifungo cha nje cha miaka mitatu na Dada Darya Dulova apewe kifungo cha nje cha miaka miwili.

Aprili 19, 2016, Ndugu Prianikov na Dada Vanera Dulova walizungumza na mwanamume fulani kuhusu Biblia. Ndugu ya mwanamume huyo aliwatuhumu Ndugu Prianikov na Dada Dulova kuwa ni wezi na kuwaitia polisi. Wote walipelekwa kituo cha polisi. Polisi walichukua alama zao za vidole na kuwanyang’anya machapisho yao.

Zaidi ya miaka miwili baadaye walikamatwa tena na kupelekwa kituoni ili kuhojiwa kwa sababu ya tukio hilo. Maofisa walichukua simu zao pamoja na hati nyingine za kibinafsi. Mkuu wa polisi alimpa profesa msaidizi wa theolojia kazi ya kuchunguza taarifa zilizokuwamo ndani ya simu za Ndugu Prianikov na Dada Dulova. Ripoti ya profesa huyo yenye kurasa 15 ilisema kwamba simu zao zilikuwa na mafundisho ya Mashahidi wa Yehova. Hatimaye kesi ya uhalifu ilianzishwa dhidi yao ikitegemea hasa ripoti hiyo. Kisha Mahakama ya Jiji la Karpinsk ikawapa ruhusa polisi kumfanya msako katika nyumba zao.

Polisi walipofanya msako katika nyumba ya Dada Dulova, walichukua vifaa vya kielekroni, vitabu, na picha. Pia walimhoji binti ya Dada Dulova mwenye umri wa miaka 18 anayeitwa Darya. Pia maofisa walifanya msako katika nyumba za ndugu zao wa kimwili pamoja na nyumbani kwa Ndugu Prianikov.

Aprili 16, 2019, kwa mara nyingine tena maofisa watatu wa Federal Security Service (FSB), mpelelezi mmoja, pamoja na maofisa wengine wawili, walivamia nyumba ya Ndugu Prianikov. Maofisa hao walichukua vifaa vyake vya kielektroni pamoja na vitu vingine vya kibinafsi.

Julai 23, 2019, Dada Darya Dulova aliitwa kituoni kwa ajili ya kuhojiwa, akiwa mtuhumiwa wa kesi ya uhalifu inayomhusu mama yake na Ndugu Prianikov. Wote watatu walituhumiwa kwa kosa la uhalifu na kesi yao ilianza kusikilizwa kuanzia Septemba 2019.

Tunasali hivi kwa uhakika kwa ajili ya hawa Ndugu na Dada zetu watatu pamoja na wengine karibu 300 wanaokabiliana na mashtaka ya kihalifu nchini Urusi: “Mungu anayetoa tumaini na awajaze ninyi shangwe yote na amani kwa kumtegemea, ili tumaini lenu liongezeke kwa nguvu za roho takatifu.”—Waroma 15:13.