Hamia kwenye habari

JANUARI 25, 2021
URUSI

Mahakama ya Rufaa ya Urusi Yaunga Mkono Uamuzi wa Kwamba Ndugu Zalipayev Hana Hatia

Mahakama ya Rufaa ya Urusi Yaunga Mkono Uamuzi wa Kwamba Ndugu Zalipayev Hana Hatia

Januari 25, 2021, Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Kabardino-Balkaria, imekataa ombi la mwendesha-mashtaka dhidi ya hukumu iliyotolewa Oktoba 7, 2020, ambapo mahakama ilitangaza kwamba Ndugu Yuriy Zalipayev hana hatia. Upande wa mashtaka unaweza kuamua kukata rufaa dhidi ya uamuzi huu pia. Hata hivyo, sasa uamuzi wa kutokuwa na hatia umeanza kutekelezwa. Mashtaka yote dhidi ya Yuriy yameondolewa. Sasa ana haki ya kudai fidia kwa kushtakiwa kimakosa.

Yuriy alimtegemea Yehova na alikuwa jasiri mahakamani ijapokuwa alijua kwamba huenda uamuzi wa mahakama wa kwamba hakuwa na hatia ukabadilishwa. Kabla tu ya hukumu kutangazwa, kwa ujasiri Yuriy aliiambia mahakama jinsi Mungu atakavyoondoa uovu wote hivi karibuni, kutia ndani mateso dhidi ya Mashahidi wa Yehova nchini Urusi. Alisema hivi: “Hata mashambulizi haya yatekelezwe kwa ubunifu kadiri gani, kuna jambo moja ambalo watesaji wanapaswa kuelewa. Hawatafanikiwa katika jitihada zao za kuvunja imani yangu katika ahadi ya Mungu kwamba hivi karibuni ataondoa uovu duniani. Ninaamini ahadi ya kwamba hivi karibuni watu kutoka mataifa yote hatimaye watatambua kwamba wao ni ndugu na dada. Hakuna jambo litakalowatenganisha. Biblia inasema hivi kumhusu Mungu: ‘Atatekeleza hukumu miongoni mwa mataifa na kunyoosha mambo kuhusiana na watu wengi. Watafua panga zao ziwe majembe ya plau na mikuki yao iwe miundu. Taifa halitainua upanga dhidi ya taifa lingine, wala hawatajifunza vita tena kamwe.’—Isaya 2:4.

“Ninaamini kwamba ahadi hii itatimizwa hivi karibuni!”