MACHI 7, 2022
URUSI
Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu Imesema Urusi Iliwanyima Mashahidi wa Yehova Haki na Uhuru Wao wa Msingi
Februari 22, 2022, Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu (ECHR) ilifanya maamuzi mawili yaliyowaunga mkono Mashahidi 15 wa Yehova. Kesi hizo zilihusu maofisa wa usalama ambao waliwadhulumu ndugu zetu walipovamia nyumba zao kati ya mwaka wa 2010 na 2012. Hukumu zilizotolewa zilionyesha kwamba Urusi ilikiuka haki ya msingi ya uhuru wa ibada wa ndugu na dada zetu. Urusi imeamriwa ilipe jumla ya zaidi ya euro 99,000 (dola 112,323 za Marekani) kama fidia. Hukumu hizo ni za mwisho na hakuna rufaa.
Hukumu hizo mbili zilizotolewa na Mahakama hiyo zilihusu kesi sita dhidi ya Urusi. a Kesi hizo zilipinga uhalali wa vibali vya kufanya upekuzi ambavyo viliwachochea maofisa wa Urusi kuvamia nyumba kadhaa na Jumba la Ufalme, kuwavua nguo ili kuwafanyia upekuzi dada wawili waliokamatwa kwa sababu ya kuhubiri, na kuchukua vitu vya kibinafsi vya wahusika. Katika visa fulani, uvamizi huo uliendeshwa na maofisa wa FSB waliojifunika uso na waliokuwa na silaha na ambao walitumia nguvu kupita kiasi walipokuwa wakishughulika na ndugu na dada zetu.
Alipokuwa akizungumza kuhusu umuhimu wa hukumu hizo, André Carbonneau, wakili wa kimataifa wa haki za kibinadamu, aliyehusishwa na idara yetu ya kisheria, alieleza kwamba hukumu hizo “zinaweka msingi muhimu sana wa kuonyesha kwamba Urusi imekuwa ikivamia nyumba za Mashahidi wa Yehova kinyume cha sheria, kutia ndani uvamizi 1,700 ambao umefanywa tangu Mashahidi wa Yehova walipopigwa marufuku mwaka wa 2017. Sasa, uvamizi wowote mpya unaofanywa kwa msingi tu wa kwamba mtu ni Shahidi wa Yehova utaonwa kuwa kinyume cha sheria na unakiuka Mkataba wa Ulaya.” Aliongeza hivi: “Ni muhimu kutaja kwamba Mahakama iliwashutumu wenye mamlaka nchini Urusi kwa kuvuruga kazi ya kuhubiri nyumba kwa nyumba. Hilo linaonyesha kwamba ECHR inaiona huduma ni utendaji wa kidini ambao wenye mamlaka hawapaswi kuvuruga.”
Ingawa maamuzi hayo mawili hayashutumu mateso ya Mashahidi wa Yehova nchini Urusi, yanaweka msingi wa maamuzi ya wakati ujao yatakayoshughulikia marufuku dhidi ya tengenezo letu. Kuna zaidi ya kesi 60 ambazo zinawahusu Mashahidi wa Yehova nchini Urusi ambazo bado hazijasikilizwa na ECHR. Tunatumaini kwamba maamuzi hayo mawili yanaonyesha jinsi Mahakama hiyo itakavyoshughulikia kesi hizo nyingine.
Tunashangilia kuona wenye mamlaka wanaoshughulikia haki za kibinadamu wakitambua utimilifu usioyumbishwa wa ndugu na dada zetu nchini Urusi. Maamuzi hayo ni uthibitisho wa kwamba Yehova anabariki jitihada za kutetea jina lake na enzi yake kuu kwa ushikamanifu.—Zaburi 26:11.
a Kesi hizo sita zilikuwa na vichwa vifuatavyo: Chavychalova v. Russia; Cheprunovy and Others v. Russia; Novakovskaya v. Russia; Ogorodnikov and Others v. Russia; Pekshuyev and Others v. Russia; na Zharinova v. Russia.