Hamia kwenye habari

MACHI 1, 2019
URUSI

Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu Yashughulikia Haraka Ombi Lililotumwa kwa Niaba ya Ndugu Aliyeteswa Urusi

Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu Yashughulikia Haraka Ombi Lililotumwa kwa Niaba ya Ndugu Aliyeteswa Urusi

Februari 25, 2019, ombi la hatua za haraka kuchukuliwa lilitumwa kwenye Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu (ECHR) kwa niaba ya Ndugu Sergey Loginov, mmoja kati ya ndugu saba walioteswa na maofisa katika jiji la Surgut lililoko eneo la magharibi la Siberia. Ndugu wengine sita walioteswa waliachiliwa, lakini Ndugu Loginov amekuwa mahabusu tangu alipokamatwa na hawezi kupata matibabu ya kutosha ya majeraha aliyopata.

Februari 26, siku moja tu baada ya ombi hilo kutumwa, ECHR ililishughulikia na kutoa uamuzi. Mahakama hiyo ilikubali ombi hilo na kuiagiza serikali ya Urusi “mara moja” imruhusu Ndugu Loginov afanyiwe uchunguzi na madaktari wa kujitegemea ili kujua kiwango cha madhara ya “kimwili na kiakili” aliyopata na kueleza ikiwa afya yake inamruhusu kuendelea kufungwa. Serikali ya Urusi imeagizwa kufanya hivyo kabla ya Machi 11, 2019.

Mahakama ya ECHR hukubali maombi kama hayo kukiwa na hali za pekee tu, wakati ambapo mtu anakabili hatari ambayo huenda ikamsababishia madhara ya kudumu. Hivyo, inatia moyo kuona kwamba mahakama ya ECHR imechukua hatua hiyo haraka sana, yaani, siku moja tu baada ya ombi kutolewa. Mahakama hiyo imeonyesha kwamba ECHR itafuatilia kwa ukaribu mateso yanayowapata ndugu zetu.

Kwa sasa, Mashahidi 19 wanakabili mashtaka ya uhalifu katika eneo la Surgut, na 3 kati yao wamewekwa mahabusu.

Kadiri tunavyoendelea kusali kwa Yehova kwa niaba ya ndugu zetu, acheni tuzingatie akilini maneno yenye kutia moyo ya Yeremia: “Amebarikiwa mtu anayemtumaini Yehova, ambaye uhakika wake uko katika Yehova.”—Yeremia 17:7.